MREMA AWAGUSA WANANCHI MLANGARINI,AAHIDI KULETA MAJI NDANI YA MIEZI SITA KILA KAYA ITAOGELEA,APANGA SIKU YA KULA BATA KILA AZINDUA KAMPENI KWA KISHINDO

Mrema Aahidi Suluhisho la Haraka Barabara na Maji Mlangarini

Na Joseph Ngilisho, ARUMERU

 

MGOMBEA udiwani wa Kata ya Mlangarini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Mrema, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo ndani ya muda mfupi endapo atachaguliwa, huku akisisitiza vipaumbele vya barabara, maji, afya, elimu, ajira na migogoro ya ardhi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ilani ya chama , leo Septemba 7,2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni zake katika Kijiji cha Manyire, Mrema  alisema barabara zote za kata hiyo zitakuwa zinapitika kwa urahisi ndani ya miezi sita, huku barabara ya Upendo akiipa kipaumbele cha pekee kwa kuwa ni kiunganishi muhimu kwa wananchi.

Changamoto ya Maji

Mrema aliahidi kusimamia upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya muda mfupi, akisema hakuna mwananchi atakayeteseka tena.

> “Ndani ya wiki moja maji yatafika mlangoni kwa kila kaya. Wananchi wa Mlangarini wataogelea kwenye neema ya maji,” alisema kwa kujiamini, huku akishangiliwa na umati wa wananchi.


Afya na Huduma kwa Vijana na Wazee

Aidha, aliahidi kuwa ndani ya miezi sita, wazee pamoja na vijana wanaofanya kazi migodini na kusumbuliwa na maradhi ya kifua watapata huduma ya madaktari maalum watakaotoa tiba bila malipo.

Ajira na Ujasiriamali

Kuhusu ajira, Mrema alisema amejipanga kuunda vikundi vya vijana vya ujasiriamali vitakavyosaidiwa kupata mikopo na elimu ya biashara ili waweze kuinua kipato chao.

Elimu na Walimu

Katika sekta ya elimu, alisema ataweka mpango mahsusi wa kuwawezesha walimu kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi ili wawe na uhakika wa kipato, hatua itakayowasaidia kutoa huduma bora kwa wanafunzi.

Migogoro ya Ardhi

Mrema aliahidi pia kusimamia suluhu ya migogoro ya ardhi katika kata hiyo kwa muda mfupi, akisisitiza kuwa kila mwenye haki atapewa haki yake bila kucheleweshwa.

Utamaduni na Burudani

Mbali na hayo, mgombea huyo alisema atahakikisha kila kijiji kinapata siku maalum ya burudani na michezo ya kitamaduni, ambapo kutakuwa na ngoma za asili, burudani za wasanii na zawadi zenye thamani kuanzia Shilingi milioni moja.

Uzinduzi huo wa kampeni uliohudhuriwa na mamia ya wananchi ulipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii waliotumbuiza na kunogesha shamra shamra hizo za kisiasa.








Ends…


Post a Comment

0 Comments