TANFOAM MARATHON YAJA KWA KISHINDO ARUSHA

 TANFOAM MARATHON YAJA KWA KISHINDO ARUSHA

Na Joseph Ngilisho – Arusha



Mashindano ya Tanfoam Marathon yamerudi kwa msimu wa pili kwa kishindo, yakipangwa kufanyika Desemba 7, 2025 jijini Arusha katika viwanja vya General Tire, huku wakazi wa ndani na wageni wa kimataifa wakihimizwa kujitokeza kushiriki na kushuhudia tukio hilo la kipekee.


Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mwenyekiti wa mbio hizo, Glorious Temu, alisema maandalizi ya mwaka huu yameboreshwa kwa lengo la kuinua vipaji vipya na kulitangaza Jiji la Arusha pamoja na Tanzania katika ramani ya michezo duniani.

“Michezo si burudani pekee, ni daraja la mshikamano, kichocheo cha afya bora na nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi kupitia utalii na uwekezaji,” alisema Temu.


Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogart Stephen, alisema Tanfoam Marathon imekuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya riadha kutokana na ubora wa maandalizi na ushiriki mkubwa.


Amesema baadhi ya wakimbiaji wa mwaka jana walipata nafasi ya kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Tokyo, Japan, jambo linalothibitisha mchango wa mbio hizo katika kukuza viwango vya riadha kitaifa na kimataifa


Mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia wakimbiaji wa kitaalamu, chipukizi na hata washiriki wa kawaida, huku Arusha ikibashiriwa kunufaika kiuchumi kupitia ongezeko la wageni, utalii na biashara.


Wananchi wa Arusha na maeneo jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo ambazo sasa zimewekwa kwenye orodha ya matukio makubwa ya michezo yanayoipa Tanzania hadhi ya kimataifa.








Ends...

Post a Comment

0 Comments