CCM Daraja Mbili Kufungua Kampeni kwa Kishindo Jumapili – “Blue House” Kuanza Mapema Asubuhi
Na Joseph Ngilisho – Arusha
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kesho, Jumapili Septemba 28, 2025, kinatarajiwa kuzindua kampeni za udiwani katika Kata ya Daraja Mbili kwa kishindo cha aina yake, katika mkutano mkubwa utakaofanyika eneo la Blue House kuanzia saa mbili asubuhi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kata ya Daraja Mbili, Shamiri Miraji Hemed, maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika huku chama kikiahidi shamrashamra na burudani tofauti kabisa na zilizozoeleka.
“Kesho tarehe 28 tunakwenda kufungua mkutano mkubwa sana katika Kata ya Daraja Mbili. Tutaweka historia kwa kufanya kampeni ambazo hazijawahi kutokea tangu kuumbwa kwa kata hii. Tutapita nyumba kwa nyumba, uvungu kwa uvungu kuhakikisha mkutano wetu unajaa na kufurika,” alisema Hemed kwa msisitizo.
🔹 Maendeleo yaliyofanyika
Aidha, Hemed aliwaomba wananchi wa kata hiyo kujiandaa pia kumpokea Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa zaidi ya wananchi 19,000 wanatarajiwa kujitokeza kumlaki na kumpa heshima kutokana na utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo inayoonekana kwa macho.
🔹 Mgombea Udiwani azungumza
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Daraja Mbili, Prosper Msofe, alisema anaamini wananchi watamrejesha kwa nafasi hiyo kutokana na kazi kubwa alizozifanya katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi.
Miongoni mwa mafanikio aliyoyataja ni pamoja na:
- Kuimarisha huduma ya maji safi
- Kudumisha ulinzi na usalama
- Ujenzi wa kituo muhimu cha afya
- Kuendeleza shule za sekondari
- Barabara za changarawe zinazorahisisha usafiri wa wananchi
Hata hivyo, Msofe alikiri kuwa bado kata hiyo haijapata hata barabara moja ya lami, hali inayosababisha vumbi katika maeneo mengi. Aliahidi kushughulikia changamoto hiyo kwa nguvu mpya endapo atapewa ridhaa nyingine.
“Kesho katika ufunguzi wa kampeni nitawaeleza kinagaubaga yale niliyoyatekeleza na yale ninayotarajia kuyafanya. Nawakaribisha wananchi wote wa Daraja Mbili kuja kusikiliza sera na vipaumbele vyetu,” alisema Msofe.
🔹 Mkutano wa kihistoria
Mkutano huo wa kesho unatarajiwa kuwa wa aina yake, ukiwahusisha wanachama wa CCM, wafuasi, wakereketwa na wananchi wote wa Kata ya Daraja Mbili. Shamrashamra za burudani, ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya na hamasa za kisiasa vinatarajiwa kuupamba mkutano huo ambao CCM imedai utakuwa wa kihistoria.
Ends..
0 Comments