KAPTENI WA NDEGE ATC AWA MGENI RASMI MAHAFALI YA 25 SHULE YA GREEN VALLEY
Na Joseph Ngilisho – Arusha
SHULE ya Msingi Green Valley yenye mchepuko wa Kiingereza jijini Arusha, imeadhimisha mahafali yake ya 25 kwa kishindo, ambapo jumla ya wanafunzi 131 wa darasa la saba wamehitimu masomo yao mwaka huu.
Mahafali hayo ambayo yalienda Sanjari na mahafali ya watoto wa pre-unit, yaliyohudhuriwa na wazazi, walimu na wageni mbalimbali, yalinogeshwa zaidi na uwepo wa mgeni rasmi, Kapteni Abdalah Rashird Abdalah, rubani wa ndege wa Shirika la Ndege la Taifa (ATC), ambaye alitumia nafasi hiyo kupongeza wahitimu na kuwatia moyo kuendelea na safari ya elimu kwa bidii na nidhamu.
Akizungumza mbele ya hadhira, Kapteni Abdalah aliwaasa wahitimu kuzingatia nidhamu na maadili mema sambamba na elimu waliyoipata.
> “Elimu bila maadili na nidhamu ni kama ndege bila usukani. Hivyo nawaomba watoto wetu mlihitimu leo mheshimu walimu, mthamini elimu mliyopewa na muwe na nidhamu kila mahali mtakapokwenda. Heshima kwa walimu wenu na wazazi wenu ndiyo itakayowafikisha mbali zaidi ya darasani,” alisema.
Aliongeza kuwa dunia ya sasa ina changamoto nyingi, hivyo nidhamu na maadili mema ni silaha pekee ya kuwavusha na kuwafanya raia wema wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Green Valley, Yahaya Njalita, alieleza furaha yake kubwa kwa shule hiyo kufikisha miaka 25 tangu kuanzishwa.
> “Kwanza namshukuru Mungu kwa kutuwezesha shule yetu kuishi na kukua kwa miaka 25 mfululizo. Hii ni historia kubwa na ushahidi wa kazi, nidhamu na mshikamano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi wetu. Tumeshuhudia kizazi baada ya kizazi kikihitimu hapa na kuendelea kufanya vizuri katika elimu na maisha,” alisema Njalita.
Aidha, Njalita aliwashukuru walimu kwa juhudi wanazoweka kila siku, pamoja na wazazi kwa kuendelea kuiamini shule hiyo, akiahidi kuwa Green Valley itaendelea kusimamia ubora na malezi bora kwa wanafunzi.
Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo kwaya, ngoma za kitamaduni na michezo ya kisanaa iliyooneshwa na wanafunzi, wakidhihirisha vipaji na ubunifu wao mbele ya wageni na wazazi.
Zaidi ya yote, mahafali hayo yalinogeshwa na ulipuaji wa fataki zilizowasha anga la jiji la Arusha, tukio lililozua shangwe kubwa kwa wanafunzi, wahitimu na wazazi, huku likiashiria furaha na heshima ya miaka 25 ya historia ya shule hiyo.
Mahafali ya mwaka huu yameacha alama isiyofutika kwa kuonyesha mshikamano wa jamii katika kuendeleza elimu bora jijini Arusha, na kuwatia moyo wahitimu kuendelea kupanda ngazi za kimaisha.
Ends...
0 Comments