Jogging ya Wazee Yafunika Kata ya Olasiti, Wazee Waking’ara na Nguvu Mpya
Na Joseph Ngilisho – Arusha
Wananchi wa Kata ya Olasiti leo waliushuhudia mtindo wa kipekee wa mazoezi ya pamoja baada ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kuandaa Jogging ya Wazee, tukio lililovutia hisia na kushangiliwa na wengi.
Jogging hiyo iliyoongozwa na Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, iliwakutanisha wazee kutoka mitaa mbalimbali ya jiji. Washiriki walikimbia umbali wa kilometa tano, kabla ya kufuatiwa na mazoezi ya viungo yaliyofanyika kwa mshikamano na furaha kubwa.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Benson Maneno alisema lengo la mazoezi hayo ni kuhamasisha wazee kujali afya zao kupitia michezo na mazoezi ya mwili.
> “Mazoezi ni tiba isiyo na gharama. Jogging hii inatufundisha kuwa umri siyo kikwazo cha kuishi maisha yenye afya bora. Ni desturi tunayopaswa kuiendeleza kila mara,” alisema Maneno.
Wazee walioshiriki jogging hiyo walionekana na furaha huku wakionyesha ukakamavu mkubwa. Baadhi yao waliwashangaza vijana waliokuwa wakishuhudia, kutokana na kasi na ujasiri waliokuwa nao.
Mzee mmoja mkazi wa Olasiti, akiwa mwenye furaha, alisema:
> “Tumejisikia vijana tena. Tunashukuru halmashauri kwa kutukumbuka na kutupa nafasi ya kufanya mazoezi haya ya pamoja.”
Kwa upande wake, Halmashauri ya Jiji la Arusha imesisitiza kuwa michezo ya aina hiyo itaendelea kuandaliwa mara kwa mara katika kata mbalimbali, ili kuhakikisha wazee wanabaki na afya bora na kuchangamsha mioyo ya jamii.
Jogging hiyo imeacha taswira ya mshikamano, afya na furaha, huku wananchi wakipongeza juhudi za jiji katika kukuza utamaduni wa michezo kwa makundi yote ya jamii.
Ends..
0 Comments