BILIONEA MULOKOZI AENDELEA KUIPAISHA MANYARA : ATENGENEZA NDEGE NYUKI KUKOMBOA WAKULIMA

BILIONEA MULOKOZI AENDELEA KUIPAISHA MANYARA: ATENGENEZA NDEGE NYUKI KUKOMBOA WAKULIMA

Na Joseph Ngilisho, Babati

Bilionea David Mulokozi kutoka mkoani Manyara ameibuka na ubunifu wa kipekee utakaosaidia wakulima, kudhibiti uwindaji haramu na kupunguza ajali za barabarani, baada ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza ndege zisizokuwa na rubani (drones) zenye teknolojia ya kisasa.


Mulokozi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mati Group Companies Limited Tanzania na Mati Technologies, alisema teknolojia hiyo inalenga kuleta mapinduzi ya kilimo na usimamizi wa rasilimali nchini. Alitoa kauli hiyo jana katika kikao cha 11 cha Baraza la Biashara mkoani Manyara.


Mapinduzi ya Kilimo


Akifafanua, Mulokozi alisema drones zinazotengenezwa kupitia Mati Technologies zina uwezo wa kufanya kazi mbalimbali shambani ikiwemo umwagiliaji, kunyunyizia dawa za kuua wadudu, kugundua magonjwa ya mazao na kutoa taarifa sahihi za dawa zinazotakiwa kutumika. Pia, ndege hizo hupima ubora wa udongo na kutoa mrejesho wa kitaalamu kwa wakulima.


“Droni hizi ni msaada mkubwa kwa mkulima kwa sababu zinapunguza gharama na kuongeza ufanisi. Kwa sasa tunazalisha kutoka Babati, tukishirikiana na wataalamu kutoka Tanzania na India. Afrika nzima, hakuna nchi nyingine inayotengeneza ndege hizi, ni Tanzania pekee,” alisema Mulokozi.


Mulokozi alibainisha kuwa mtaji wa awali wa mradi huo umefikia dola milioni 2 za Marekani, sawa na shilingi bilioni 5–6 za Kitanzania. Aliongeza kuwa kila droni itauzwa kwa takribani shilingi milioni 17 baada ya kumalizika majaribio ya matumizi.


Udhibiti wa Uwindaji Haramu na Ajali


Mbali na matumizi ya kilimo, Mulokozi alisema teknolojia hiyo pia inalenga kusaidia kulinda wanyamapori kwenye maeneo yenye uwindaji haramu kwa kutumia drones za surveillance.


Aidha, alisema wamefanya utafiti wa kina kwa kushirikiana na kampuni kutoka Ubelgiji kuhusu matumizi ya kamera maalum za kudhibiti ajali za barabarani. Kamera hizo zitafungwa katika maeneo hatarishi nchini na zitagharimiwa na kampuni yake, huku serikali ikinufaika moja kwa moja na mapato yatakayotokana na faini za makosa ya madereva.


“Tumezungumza na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu mpango huu. Serikali haitaingia gharama yoyote. Madereva watakaokutwa na makosa watalipa faini papo hapo, na mapato hayo yataigawanya serikali na Mati Technologies. Baada ya kufunga kamera hizi, makusanyo ya serikali yataongezeka kwa zaidi ya asilimia 1000,” alisisitiza Mulokozi.


Mulokozi alikadiria uwekezaji wa mradi huo wa kamera kufikia shilingi bilioni 500, akisisitiza kuwa utakuwa suluhisho la kudumu la kupunguza ajali na kuongeza usalama barabarani.

Ends ..

Post a Comment

0 Comments