MWALIMU MKUU NGARENARO ARUSHA MBARONI KWA KUMFUNGA MINYORORO MWANAFUNZI WAKE ILI ALALE DARASANI USIKU ,POLISI WARUKA UKUTA KUMWOKOA ,TAZAMA PICHA

MWALIMU MKUU, MLINZI WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA UKATILI DHIDI YA MTOTO

Na Joseph Ngilisho, Arusha



Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngarenaro, Bw. Mussa Luambano (50), na mlinzi wa shule hiyo, Bw. Olais Mollel (33), kwa tuhuma za ukatili dhidi ya mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 13 (jina limehifadhiwa).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 3, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 1, 2025, ambapo inadaiwa watuhumiwa walimfunga mwanafunzi huyo mguu kwa kutumia mnyororo kwenye dawati na kisha kumfungia ndani ya darasa kwa madai ya kuwa ni mtoro.


Kamanda Masejo alibainisha kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.


Akizungumzia tukio hilo kwa niaba ya sekta ya elimu, Mkurugenzi wa Elimu Jiji la Arusha,  Rehema Ng’wasi, alilaani vikali kitendo hicho akikitaja kuwa ni kinyume na maadili ya kazi ya ualimu na haki za mtoto. “Ni jambo la kusikitisha na halikubaliki hata kidogo. 


Walimu na watumishi wa shule wanapaswa kuwa walinzi wa usalama wa watoto, siyo chanzo cha mateso. Tumeunda timu maalum ya uchunguzi wa kiidara na tutachukua hatua stahiki za kinidhamu sambamba na taratibu za kisheria,” alisema.


Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeendelea kuwataka wananchi kufichua matukio ya ukatili na uhalifu katika jamii ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika kukiuka sheria.


Ends...

Post a Comment

0 Comments