TUCTA Yazindua Jengo la Biashara Arusha, Waziri Ridhiwani Apongeza Hatua ya Uwekezaji
Na Joseph Ngilisho-Arusha
CHAMA Cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kimezindua rasmi jengo jipya la biashara jijini Arusha, ikiwa ni hatua kubwa ya kujitegemea kifedha na kuwekeza katika miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wanachama wake na jamii kwa ujumla.
Uzinduzi huo umefanyika leo agosti 15,2025 katika eneo hilo lililopo katikati ya jiji la Arusha, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ridhiwani Kikwete. Tukio hilo limehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa TUCTA, wawakilishi wa vyama shiriki, viongozi wa serikali, na wadau wa sekta ya kazi na ajira.
Akizungumza wakati wa kuzindua jengo hilo, Waziri Ridhiwani aliipongeza TUCTA kwa kuonesha mwelekeo mpya wa uendelevu wa kifedha na kuwekeza katika vitega uchumi vinavyoleta tija kwa wafanyakazi na taifa.
“Ujenzi wa jengo hili sio tu unaonesha ubunifu wa viongozi wa TUCTA, bali pia ni ushahidi kwamba vyama vya wafanyakazi vinaweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi. Hii ni njia ya kupunguza utegemezi na kujenga uhuru wa kifedha wa chama,” alisema Ridhiwani.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na TUCTA kuhakikisha kuwa haki na maslahi ya wafanyakazi yanazingatiwa, sambamba na kuhamasisha uwekezaji unaochangia pato la taifa.
Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alisema mradi huo wa jengo ni sehemu ya mkakati mpana wa chama wa kuanzisha vitega uchumi vinavyodumu na kwamba kupitia uwekezaji huo watakuwa na uwezo wa kukusanya zaidi ya sh, milioni 50 kwa mwezi.
“Tumepanga kujenga misingi imara ya kifedha kwa TUCTA kupitia miradi ya maendeleo kama hii. Tunataka wanachama wetu waone matunda ya michango yao, lakini pia chama kiwe na nguvu ya kujitegemea bila kutegemea misaada,” alisema Nyamhokya.
Aliongeza kuwa mapato yatakayopatikana kutokana na jengo hilo yatasaidia kugharamia shughuli za kiutendaji, mafunzo kwa wafanyakazi, na miradi ya kijamii inayolenga kuwanufaisha wanachama.
Jengo lenye thamani kubwa
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, jengo hilo la kisasa lina ghorofa kadhaa na limejengwa kwa viwango vya kimataifa, likiwa na sehemu za ofisi, maduka, na kumbi za mikutano.
Aidha, jengo hilo linatarajiwa kuongeza ajira kwa wakazi wa Arusha kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara zitakazofanyika humo.
Mmoja wa wanachama wa TUCTA aliyeshuhudia uzinduzi huo, Bw. Emmanuel Mushi, alisema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa chama hicho.
“Hii ni ishara kuwa chama chetu kinawajali wanachama. Sasa tunaona fedha zetu zikitumika kuleta maendeleo na siyo tu kwenye mazungumzo ya madai ya mishahara,” alisema Mushi.
Faida kwa jamii ya Arusha
Mbali na TUCTA kunufaika moja kwa moja, jengo hilo litakuwa na mchango wa kiuchumi katika jiji la Arusha kwa kuongeza mapato ya kodi, kutoa nafasi za ajira, na kuchochea biashara za ndani.
Wadau wa sekta binafsi pia wameonesha nia ya kulipangisha jengo hilo kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hatua itakayoongeza mapato ya chama na kuchochea ushindani wa kibiashara katika eneo hilo.
Hata hivyo jumla ya vyama 16 vinavyounda TUCTA vimepokea zawadi ya vyeti akiwemo Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi waandishi wa habari JOWUTA Mussa Juma.
Sanjari na hayo wametambua mchango wa wadau muhimu waliounga mkono juhudi zao za maendeleo ya kukakamilisha jengo hilo akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim kwa ushirikiano na mchango wake mkubwa kuhakikisha wanafikia mafanikio makubwa ya shirikisho.
Uzinduzi wa jengo la TUCTA jijini Arusha ni hatua inayodhihirisha dira mpya ya vyama vya wafanyakazi nchini katika kushiriki moja kwa moja kwenye ujenzi wa uchumi wa taifa. Wadau wengi wameeleza kuwa hatua hiyo ni mfano wa kuigwa na vyama vingine, hususan katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inawanufaisha wanachama wake na jamii kwa ujumla.
Ends..
0 Comments