Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
JESHI la Polisi mkoa wa Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya kijana Wilson Mbise (25), mkazi wa kijiji cha Muungano, Kata ya King’ori, wilayani Arumeru.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Jumamosi katika eneo la Msitu wa Mazingira, likihusisha kundi la watu wanaodaiwa kujichukulia sheria mkononi.
Mashuhuda wa kijiji hicho wanasema kuwa marehemu alikuwa na wenzake wanne wakati waliposhambuliwa na kundi kubwa la watu waliokuwa na silaha za jadi.
Mbali na mauaji ya Mbise, vijana wengine Daud William (17), Kelvin Humphrey (22), Godbless Emmanuel (30) na Allen Nanyaro (21) walijeruhiwa vibaya na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa matibabu.
MANUSURA WA TUKIO HILO ASIMULIA VIBOKO 70 VILIVYOUA RAFIKI YAKE ARUSHA
Kijana anayefahamika kwa jina la Paulo Mbise mkazi wa kata King’ori wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, akielezea tukio la wao kuadhibiwa viboko kwa tuhuma za wizi wa mahindi kiasi cha wastani wa gunia moja, kiasi cha mwenzao kufariki dunia wilayani humo.
Akizungumza akiwa kwenye maumivu makali, amesema akiwa na wenzake wanne walikamatwa na kuvuliwa nguo na kuchapwa viboko bila kikomo wakitakiwa kueleza ni wapi yalipo mahindi yanayodaiwa kuibiwa shambani katika eneo hilo.
Aidha, Paulo amesema wakiwa wanaendelea kuchapwa, mwenzao anayefahamika kwa jina la William Sarakikya alifariki dunia akiwa achapwa huku amening'inizwa kwenye mti na baadaye alifariki dunia lakini waliendelea kumchapa wakisema anajifanya amekufa.
"Baada ya kuona wakiendelea kumchapa bila kutikisika waliona amekufa na wao walianza kukimbia mmoja baada ya mwingine, wakati hayo yakiendelea nilikuwa nikishuhudia kwa macho yangu yafiki yangu akikata roho"Alisema Paul
Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, ACP Salvas Makweli, amesema tayari watu sita wanashikiliwa kuhusiana na mauaji hayo huku upelelezi ukiendelea.
“Ni kweli tumewakamata watuhumiwa sita. Kwa sasa majina yao tunayahifadhi hadi taratibu za kisheria zitakapokamilika. Hatuwezi kuvumilia vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio chochote,” alisema ACP Makweli.
Mwili wa marehemu Mbise umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu kabla ya kuzikwa.
Onyo kwa wananchi:
ACP Makweli ametoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kulipiza kisasi na badala yake kuwafikisha watuhumiwa wa makosa mikononi mwa vyombo vya dola.
“Jeshi la Polisi litahakikisha kila atakayebainika kuhusika na tukio hili anafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
Kwa sasa, watuhumiwa wanasubiri hatua za kisheria huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini chanzo halisi cha mzozo uliopelekea tukio hilo. Polisi wameahidi kutoa taarifa zaidi pindi zitakapokamilika.
Ends...
0 Comments