KUMBUKUMBU YA SHEIKH SALIM DARUWESHI: WAUMINI TWARIQA KUFANYA DUA MAALUMU KUOMBEA AMANI UCHAGUZI MKUU
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
WAUMINI wa taasisi ya Twariqa na mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kujumuika Jumatano ijayo, Agosti 21, 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa kiongozi mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Salim Daruweshi(Mti Mkavu).
Sheikh Daruweshi, aliyefariki dunia Agosti 21, 2024, aliheshimika kwa mchango wake mkubwa katika malezi ya kiroho na mshikamano wa kijamii, akibaki katika nyoyo za waumini wake kama kiongozi aliyehimiza mshikamano, amani na mshikikano wa kitaifa.
Sherehe hizo za kumbukumbu zitafanyika katika makao makuu ya taasisi ya Twariqa, ambapo mbali na dua ya kuombea roho ya marehemu, kutasomwa pia dua maalumu ya kuombea amani ya Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 16,2025,Sheikh Mubaraka Salim, mmoja wa viongozi wa juu wa taasisi hiyo, alisema kumbukumbu hiyo inalenga kuenzi maono ya marehemu Sheikh Darueshi.
“Sheikh Daruweshi aliamini katika mshikamano wa Watanzania wote bila kujali tofauti za dini au kisiasa. Dua hii maalumu ni mwendelezo wa ujumbe wake wa kudumisha mshikamano na kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu,” alisema Sheikh Mubaraka.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Twariqa,Halifa Omary Said alisema maadhimisho hayo yatakutanisha Zawia zote za taasisi katika kuliombea Taifa amani kuelekea uchaguzi Mkuu ,kuwaleta viongozi pamoja.
"Katika kuelekea maadhimisho hayo tunatarajia kushiriki masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu ,utunzaji wa mazingira na tunaenzi yale mema aliyokuwa akituasa ambayo ni mshikamano na mahusiano mema"Alisema.
Naye katibu wa Twariqa jumuiya ya wanawake , Rehema Athumani, aliwakaribisha waumini wote wa taasisi hiyo kujumuika pamoja katika kumbukizi la maadhimisho hayo yatakayofanyika agosti 21,2025 Zawia Kuu Arusha.
“Marehemu alikuwa akisisitiza kila mara kwamba amani ni zawadi ya Mungu ambayo kila Mtanzania anapaswa kuilinda. Tunashukuru kuona taasisi na waumini wakiendeleza misingi aliyoacha,” alisema kwa hisia.
Katika maadhimisho hayo, viongozi wa dini na kijamii kutoka maeneo mbalimbali wanatarajiwa kushiriki, huku wakiungana na waumini kufanya ibada za pamoja. Aidha, kutakuwa na mihadhara itakayogusia umuhimu wa mshikamano wa kitaifa, mshikikano wa dini na heshima kwa amani ya taifa.
Sheikh Daruweshi alitambulika pia kwa harakati zake za kijamii ikiwemo kusaidia watoto yatima na vijana wasio na ajira kupitia miradi ya kujitegemea, hatua iliyomfanya apate heshima kubwa hata nje ya mipaka ya nchi.
Dua hiyo ya kumbukumbu inatarajiwa kukutanisha maelfu ya waumini na wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwa pia ni ishara ya mshikamano kuelekea kipindi cha kisiasa kinachotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ends.....
0 Comments