Monduli Yazizima: Mamia Wamsindikiza Kadogoi Kuchukua Fomu ya Ubunge
Na Joseph Ngilisho- MONDULI
Monduli – Mamia ya wananchi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Monduli, leo Agosti 26,2025 walijitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wao, Isack Joseph Capriano maarufu kwa jina la Kadogoo, wakati akichukua fomu ya kugombea ubunge.
Msafara huo ulijaa nderemo, vifijo na nyimbo za jadi huku sehemu kubwa ya waliohudhuria wakiwa ni wananchi wa jamii ya kifugaji waliovalia mavazi ya kimasai na kubeba fimbo za asili, jambo lililofanya tukio hilo kuvutia zaidi.
Wananchi walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha jina la Kadogoo, wakidai kuwa ni kiongozi anayejua shida zao na ni sauti ya kweli ya Monduli.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Kadogoo alimshukuru Rais Samia na chama chake kwa imani waliyoonyesha kwake. Aliahidi kuwaletea wananchi ushindi wa kishindo na kuongeza kura za urais kwa kiwango kikubwa.
> “Ninamshukuru sana Rais Samia kwa kuniamini tena. Naahidi kuwa kura za urais Monduli zitavuka 120,000. Hii ni dhamira yangu na dhamira ya wananchi wenzangu,” alisema Kadogoo huku akishangiliwa.
Ameeleza kuwa wananchi wa Monduli hawatakuwa na majuto wakimchagua, kwani alipokuwa Mwenyekiti wa Halmashauri alishiriki kusimamia vema miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa sasa, ameahidi kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa vitendo.
> “Nawashukuru sana wananchi wa Monduli. Najua mmeacha shughuli zenu na wengine mmetoka mbali kwa ajili yangu. Sina maneno mazuri ya kutosha, ila niseme tu Asanteni sana,” aliongeza kwa bashasha.
Wananchi waliohudhuria walimpongeza Kadogoo wakisema ni kiongozi shupavu na mchapakazi ambaye amewahi kuthibitisha uwezo wake katika uongozi wa halmashauri. Walisema kuwa wanatarajia mabadiliko makubwa endapo atapewa nafasi ya kuliongoza jimbo hilo bungeni.
Wamesema mgombea huyo amefika kila kata, kushughulikia migogoro ya ardhi na kero mbalimbali za wananchi, jambo linaloonesha kwamba ni kiongozi wa vitendo. Maelfu waliovalia rangi za kimasai na kushiriki katika msafara walimsindikiza Kadogoo hadi ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wakionyesha imani yao na mshikamano wao na mgombea wao wa CCM.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe, alisema Kadogoo ni kiongozi anayejali wananchi wake. “Monduli imepata kiongozi anayejitoa kwa wananchi na ambaye anafahamu changamoto zao. Kadogoo ni mchapa kazi,” alisema Mwaisumbe.
Miongoni mwa wananchi waliomsindikiza, Naserian Kaika, alisema Kadogoo ndiye kiongozi pekee anayeweza kulipigania jimbo la Monduli ipasavyo.
> “Kadogoo anatufahamu vizuri, amekuwa kiongozi wetu kwenye halmashauri na tunaona matunda yake. Sisi hatuna shaka naye, Monduli iko salama mikononi mwake,” alisema Naserian.
Kwa upande wake, Mzee Saitoti Ole Nangishu mmoja wa wazee wa kimila, alisema jamii ya kifugaji ina imani kubwa na Kadogoi kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo vijijini.
> “Tumemlea, tumemfundisha mila na desturi za Kimaasai, na sasa tunamkabidhi jimbo. Tunaamini atakuwa mwakilishi wa kweli bungeni,” alisema Mzee Saitoti.
Vijana pia walionyesha mshikamano mkubwa. Lazaro Parmena, kijana wa Monduli, alisema wako tayari kuhakikisha Kadogoi anashinda kwa kishindo.
> “Sisi vijana tuko nyuma yake kwa asilimia mia moja. Kadogoi anaijua Monduli kuliko mtu yeyote, na tunaamini atasimamia ajira na maendeleo yetu,” alisema.
Ends..
0 Comments