By arushadigtal-Dar
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebatilisha uteuzi wa Luhaga Mpina kama mgombea wa urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo, ikisema hakufuata taratibu za chama hivyo. Uamuzi huu unajiri baada ya kiongozi wa chama na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala, kulalamikia kupitishwa kwa Mpina kinyume na kanuni za chama.
Mpina amekutana na kadhia hiyo siku moja kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya uteuzi wa wagombea wa udiwani, ubunge na urais kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Hatua hiyo inafuata taratibu za kuweka mapingamizi dhidi ya mgombea, ambayo yanaweza kufanywa na mgombea mwingine, msajili au Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mwisho wa kuweka pingamizi ni Agosti 28, saa 10:00 jioni, isipokuwa ikitolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa kipindi cha siku 14 baada ya uteuzi.
Mpina na mgombea mwenza wake, Fatma Fereji, tayari walichukua fomu za INEC na wanatarajia kuzirejesha kesho, Agosti 27, kwa ajili ya uteuzi. Wawili hao pia wamezunguka mikoani wakikusanya wadhamini 200 katika kila mkoa, ikiwemo mikoa miwili ya Zanzibar.
0 Comments