KEMBAKI AKUBALI YAISHE AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUMWAMINI,ASEMA UONGOZI NI KUPOKEZANA

Na Arushadigital-TARIME

 Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini na mtia nia wa nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa 2025, Michael Kembaki, amevunja ukimya baada ya jina lake kuondolewa na vikao vya juu vya uteuzi vya chama hicho.


Kembaki, ambaye katika kura za maoni aliongoza kwa kupata kura 1,572, amesema kuwa anakubaliana na maamuzi ya chama licha ya jina la mgombea mwingine kupitishwa badala yake ambaye ni Ester Matiko.



Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kembaki amesema:

 "Nawashukuru sana wananchi wa Tarime kwa kuniamini na kunipa kura zenu, lakini kama mnavyojua, utaratibu wa chama chetu hauishii kwenye kura za maoni pekee. Mgombea hupatikana kupitia mchakato wa vikao mbalimbali vya chama."


Akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa nafasi aliyopewa kulitumikia Taifa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Kembaki alisisitiza kuwa uongozi ni kupokezana.


"Mwaka 2020 nilikuwa wa pili kwenye kura za maoni lakini nikaaminiwa kupeperusha bendera ya chama. Safari hii niliyepata kura nyingi sikuteuliwa, lakini nimepokea maamuzi ya chama kwa mikono miwili," amesema.


Aidha, Kembaki amewaomba wafuasi wake kuvunja makundi na kumuunga mkono mgombea aliyeteuliwa:

 "Nawaomba wanachama wenzangu, mashabiki wangu na wananchi wa Tarime tuvunje makundi yote. Mgombea ameshapatikana, kilichobaki ni kumnadi kwa nguvu zote ili tushinde kwa kishindo," amesisitiza.



Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, amesema zaidi ya asilimia 85 ya ahadi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita tayari zimetekelezwa, huku fedha nyingi zikiletwa wilayani humo kwa idhini ya Rais Samia.


Kembaki amekumbusha kuwa mwaka 2020 licha ya kupata kura 64 dhidi ya zaidi ya kura 200 za mpinzani wake, bado CCM ilimteua kuwa mgombea, jambo linalomfanya kuamini kuwa chama hakina upendeleo bali kinasimamia misingi imara ya haki na maadili.


Amehitimisha kwa kuahidi kushirikiana kikamilifu katika shughuli za chama na maendeleo ya jimbo:

 "Nitashiriki shughuli zote za maendeleo. Sasa ni muda wa umoja na maelewano. Chama kina utaratibu mzuri wa kupata wagombea; tuendelee kuamini kuwa huu ni mchakato unaolinda heshima ya CCM."

Ends..

Post a Comment

0 Comments