ALIYEWATAJA MAPAPA WA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA,YAMKUTA AFUNGWA MAISHA JELA

Na Arushadigtal 


MSHTAKIWA Abdallah Chande aliyeomba nafuu mahakamani akidai amekuwa msaada mkubwa, akitaja majina ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya Kigamboni na Afrika Kusini, amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kusafirisha dawa hizo.


Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Monica Otaru ilimtia hatiani Chande na Chrispin Francis baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin pasi na kuacha shaka.


Akisoma hukumu, Jaji Otaru alisema kuwa Juni 5 mwaka 2021, polisi walipokea taarifa alikokuwa mshtakiwa Chande, alikuwa anatafutwa kwa shauri la dawa za kulevya mkoani Morogoro.


Alisema polisi walikwenda Tegeta wakamkamata. Katika harakati za kumpeleka Morogoro walipokea taarifa alipokea dawa zingine na dawa hizo zilihifadhiwa wa Chrispin.


Mshtakiwa Chande alionesha maeneo ya Kinondoni Manyanya au Tegeta ambapo mshtakiwa Chrispin anaweza kupatikana.


Juni 10, 2021 mshtakiwa wa pili alipatikana Kinondoni Manyanya, alikiri kupokea dawa za kulevya kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza Chande.


"Mshtakiwa wa pili aliwapeleka askari Kimara kwenye nyumba ya mzazi mwenzake, walipofika alikwenda nyuma sehemu ya kutupa taka, alipochimba ilikutwa ndoo yenye pakiti tisa za dawa aina ya heroin kilo 7.73, wakashtakiwa kwa kusafirisha dawa," alisema Jaji Otaru.



Alisema katika kuthibitisha upande wa mashtaka uliita mashahidi saba na vielelezo vinane ambapo Mkemia alipofanya uchunguzi ilibainika kuwa ni heroin kilo 7.73.


Mshtakiwa wa kwanza alipojitetea alidai alikamatwa nyumbani Tegeta Ununio kwa shauri la kusafirisha dawa za kulevya lililokuwa mkoani Morogoro, alikana kumfahamu mshtakiwa wa pili na kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya.


Akijitetea mshtakiwa wa pili alidai alikamatwa Kinondoni kwa shtaka la bangi na si heroin na kwamba hizo bangi hazikuwa zake walipita watu wakaangusha.


"Nimezingatia hoja za pande zote mbili , nimezingatia sheria inataka Jamhuri kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka, mimi nisiwe na shaka hata kidogo ninapotoa hukumu.


"Katika kuangalia iwapo washtakiwa wana hatia au la nilijipa maswali kadhaa na majibu kutokana na ushahidi ni kwamba kilo 7.73 ni dawa za kulevya aina ya heroin, mshtakiwa wa kwanza hakukutwa na dawa, lakini yeye ndiye aliyesema dawa zipo kwa mshtakiwa wa pili.



"Mshtakiwa wa pili ndiye aliyewapeleka wapelelezi zilikokuwa dawa, sina sababu ya kutowaamini mashahidi wa Jamhuri kuwa mshtakiwa wa kwanza alimtaja mshtakiwa wa pili na mshtakiwa wa pili aliwapeleka zilikokuwa dawa akachimba.


"Mshtakiwa wa kwanza alikuwa na ufahamu kuhusu dawa japo hakukutwa nazo. Sheria si lazima ukutwe nazo, lakini lazima uwe na ufahamu," alisema Jaji.


Alisema washtakiwa wote walihusika, upekuzi ulifanyika kwa kufuata utaratibu, mpokezano wa kielelezo ulifuata sheria na utaratibu.


"Baada ya kusema hayo mahakama inaona upande wa mashtaka wamethibitisha shtaka bila kuacha shaka, inawatia hatiani washtakiwa wote wawili kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya," alisema Jaji Otaru.


Baada ya kuwatia hatiani upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mafuru Moses na Erick Kamala, waliomba washtakiwa wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria, kiwango cha dawa walichokutwa nacho ni kubwa na zina madhara makubwa kwa afya, yanachochea uhalifu, vijana kuwa mateja na serikali kukosa nguvu kazi.



Akiomba nafuu ya mahakama, mshtakiwa wa kwanza Abdallah alidai tangu siku ya kwanza amekuwa msaada mkubwa kwa nchi, kataja majina ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliopo Kigamboni na Afrika Kusini.


Alidai kwa kutoa taarifa hizo aliona madhara, hivyo aliomba mahakama wakati ikitoa adhabu iangalie na msaada aliotoa.


Mshtakiwa huyo pia alidai anaumwa kisukari kipindi chote na ana watoto wanamtegemea.


Mshtakiwa wa pili Chrispin aliomba mahakama izingatie muda aliokaa gerezani, familia inategemea, mgonjwa wa UTI wa mgongo anatibiwa MOI, alitoa vyeti kuthibitisha matibabu yake.


Akitoa adhabu Jaji Otaru alisema kuwa kwa kazingatia maombolezo ya pande zote mbili, kutokana na madhara ya dawa za kulevya kwa raia na taifa, adhabu yake kisheria ni kifungo cha maisha gerezani.



"Kutokana na hayo mahakama inawahukumu washtakiwa wote na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani," alisema Jaji Otaru.


Aliamuru magereza kuzingatia matibabu ya washtakiwa kwa kuwa ni wagonjwa na kuamuru kielelezo cha dawa za kulevya kiharibiwe.

Post a Comment

0 Comments