TANAPA YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO ,YAZAWADIA MAMILIONI KWA ASKARI WAKE WALIOFANYA VIZURI KWA ULINZI WA RASILIMALI

Na Joseph Ngilisho- MANYARA


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limepata mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato yake, yaliyotokana na weledi wa Watumishi wake wakiwemo askari wa uhifadhi na kufanikiwa kukusanya  kiasi cha Sh. bilioni 500 kati ya Sh. bil.430 iliyokusudiwa katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Kuji, akizungumza jana katika siku ya maadhimisho ya askari wanyamapori duniani,(World Ranger Day) iliyofanyika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, amesema katika makusanyo hayo wamevuka lengo kwa kukusanya zaidi Sh.bil.70.

"Mwaka uliopita wa 2024/25, Shirika letu lilifanikiwa kukusanya takribani bilioni 500, wakati bajeti yetu tulikasimiwa kukusanya takribani shilingi bilioni 430. Kwa hiyo tumevuka lengo kwa kukusanya bilioni 70 na hii imetokana na weledi wa askari wetu kusimamia vizuri mapato ya mageti ya kuingilia"

"Hapo mwanzo kabla hatujaingiliwa na ugonjwa wa UVIKO 19, watumishi wetu, tuliamua wapewe posho au motisha, baada ya kuvuka malengo ya makusanyo. Wakati huo tulikuwa tukipata motisha mshahara wa mwezi mmoja.”Alisema Kuji

Akiongelea maadhimisho hayo yaliyoambatana na gwaride maalum na maonesho ya vifaa vya kisasa vya Tehama na Magari ya doria lililofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, mkoani Manyara,Kuji aliwataka  askari wa uhifadhi nchini kuongeza uadilifu, nidhamu,Weledi  na uwajibikaji katika kulinda rasilimali za taifa.

Pia  alisisitiza kuwa mafanikio ya uhifadhi nchini hayawezi kupatikana bila askari kuzingatia maadili ya kazi na kuwa waaminifu katika majukumu yao.

>

“Askari wa wanyamapori ni uti wa mgongo wa juhudi za uhifadhi nchini. Tunahitaji askari wenye uadilifu, walio tayari kulinda hifadhi zetu kwa moyo wa kizalendo na kutojihusisha na vitendo vya rushwa au kushirikiana na majangili,” alisema Kamishna Kuji.


Aliongeza kuwa TANAPA itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya askari watakaobainika kwenda kinyume na maadili ya kazi, huku akiwataka wote kuendelea kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.

Maadhimisho ya mwaka huu yaliambatana na kaulimbiu isemayo "Rangers, Powering Transformative Conservation", ikieleza nafasi muhimu ya askari wa wanyamapori katika kuleta mabadiliko chanya ya uhifadhi, ikiwemo kukabiliana na ujangili, uharibifu wa mazingira na usimamizi wa maliasili.

Maadhimisho hayo yalipambwa na gwaride la heshima kutoka kwa askari wa TANAPA waliotoka katika hifadhi mbalimbali nchini. Aidha, askari waliofanya kazi kwa weledi na kujitolea wakiwa kazini walitunukiwa vyeti vya heshima na fedha taslimu, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao kwa taifa.

Zaidi ya askari 40 walitambuliwa kwa utendaji bora, ambapo wengine walipewa zawadi maalum za fedha tasilimu na vyeti kwa kushiriki katika oparesheni za hatari za kuokoa wanyamapori, wageni wa hifadhi, na mali zilizokuwa hatarini.

Kamishna Kuji alisema kuwa kuanzia sasa shirika hilo litakuwa na utaratibu maalumu wa kuwazawadia askari wake wanaofanya vizuri katika ulinzi wa rasilimali za taifa pamoja na ulinzi wa mapato kwenye mageti ya kuingilia wageni.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Dkt. Robert Fyumagwa, alitoa wito kwa jamii na wadau wa uhifadhi kuendelea kushirikiana na askari wa hifadhi katika kulinda urithi wa taifa.

>

“Tunatambua mchango mkubwa wa askari wetu wa wanyamapori. Ni jukumu la kila Mtanzania kuwathamini na kuwaunga mkono, kwani wao ndio wanaolinda utalii, mazingira na rasilimali kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Dkt. Fyumagwa.


Aidha, aliahidi kuwa TANAPA itaendelea kuboresha maslahi ya askari na mazingira yao ya kazi ili kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto wanazokutana nazo wakiwa kazini.

TANAPA itaendelea kuwatambua na kuwapongeza askari wanaolinda urithi wa taifa kwa ujasiri na kujitolea. Shirika hilo limedhamiria kuimarisha nidhamu, kuondoa mianya ya rushwa na kushirikiana kwa karibu na jamii ili kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unaendelea kuwa wa mfano barani Afrika.

Ends. ....

Post a Comment

0 Comments