Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
ARUSHA – Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ameahidi kusimamia kwa nguvu zote ukuzaji wa sekta ya utalii, uchumi pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo, huku akisisitiza kuwa Arusha itaendelea kuwa kinara wa utalii nchini.
Makalla alitoa kauli hiyo leo Agosti 29,2025, muda mfupi baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kupokelewa kwa shamrashamra na mamia ya wananchi wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Missaile Albano Musa, asubuhi ya leo Agosti 29, 2025.
Akizungumza mbele ya wananchi na wadau wa sekta mbalimbali, RC Makalla alisema Arusha ni mkoa wa kipekee ambao serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeupa kipaumbele kutokana na nafasi yake ya kimkakati katika kukuza pato la taifa kupitia utalii.
> “Arusha ni Mkoa mzuri na wa kimkakati, ni Mkoa wa Kiutalii. Lengo la serikali, kuanzia kwa Rais wetu, ni kukuza utalii. Natawahakikishia wadau wote wa utalii na wananchi kwa ujumla kuwa kwa maarifa na uzoefu nilionao, Mkoa wa Arusha utaendelea kuwa kinara wa utalii nchini,” alisema Makalla.
Katika salamu zake, RC Makalla alisisitiza kutoridhishwa na tabia za uzembe miongoni mwa baadhi ya watumishi wa umma, akisema serikali inataka kuona wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
> “Sitavumilia uzembe wa aina yoyote katika kuwatumikia wananchi. Arusha inahitaji viongozi na watendaji wenye moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi,” aliongeza.
Mkuu huyo wa mkoa pia aliwashukuru viongozi wa dini kwa mapokezi yao mazuri na akawataka kuendeleza mshikamano wa kijamii. Alisisitiza kuwa ulinzi wa amani na utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya kila mmoja na mkoa kwa ujumla.
> “Ninashukuru sana viongozi wa dini kwa mapokezi yenu. Nasisitiza tushirikiane kulinda amani na mshikamano, kwani bila amani hakuna maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu,” alisema RC Makalla.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mapokezi hayo walimpongeza RC Makalla kwa maneno yake ya kuahidi uwajibikaji na kukuza sekta ya utalii, wakisema wana imani kubwa kuwa uongozi wake utaleta mabadiliko chanya.
Ends...
0 Comments