DC-TUMAINI JUNIOR SCHOOL INATUHESHIMISHA KARATU,AAHIDI USHIRIKIANO NA SHULE BINAFSI ,MKURUGENZI AFICHUA SIRI YA MAFANIKIO

Serikali Yaahidi Kuendeleza Ushirikiano na Shule Binafsi Karatu

Na Joseph Ngilisho-KARATU

Karatu – Serikali wilayani Karatu imeahidi kuendelea kuiunga mkono shule binafsi ya Tumaini Junior School, ambayo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma na kushika nafasi za juu katika matokeo ya mitihani ya kitaifa, kimkoa na kitaifa, ili kuhakikisha inaendelea kutoa elimu bora zaidi na kuiletea heshima wilaya hiyo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dkt. Lameck Karanga, wakati wa mahafali ya 15 ya kuhitimu darasa la saba kwa wanafunzi 78 wa shule hiyo, pamoja na wanafunzi 14 wa elimu ya awali kutoka Tumaini TX.

Akizungumza leo agosti 30,2025  katika mahafali hayo, Dkt. Karanga alizitaka shule nyingine binafsi na za umma kuiga mfano wa shule ya Tumaini Junior, huku akiahidi kuwa serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana na taasisi zote zinazofanya vizuri kielimu.

“Sisi kama serikali jukumu letu ni kuwaunga mkono wadau wa elimu, hasa sekta binafsi, na kuhakikisha tunaonesha ushirikiano mkubwa kwao. Kama mnavyofahamu, Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameweka sera ya elimu bure kwa wanafunzi wote, na sisi tunapaswa kuhakikisha tunaunga mkono juhudi hizo,” alisema Dkt. Karanga.


Aidha, kiongozi huyo alisisitiza wajibu wa wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora, akiwataka hasa wazazi kutoka jamii za kifugaji wilayani humo kuacha mtazamo wa kuwatumia watoto kuchunga mifugo au kuwaoza kwa tamaa ya mali.

“Wito wangu ni kuhakikisha wazazi wanaleta wanafunzi shule. Elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” aliongeza.


Awali, Mkurugenzi wa Shule ya Tumaini Junior na Tumaini TX, Modest Bayo, alisema siri ya mafanikio ya shule hiyo ni mshikamano na ushirikiano wa karibu baina ya walimu ,wazazi na wanafunzi.

“Mkakati wetu kwa sasa ni kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi katika ufaulu wa kitaifa. Tuna walimu wenye ari na moyo wa kujituma, jambo linalotuwezesha kila mwaka kuwa miongoni mwa shule bora kitaifa,” alisema Bayo.

Aliongeza kuwa shule hiyo inajivunia kuwa na walimu wenye uwezo mkubwa wa kufundisha, huku akimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kutoa motisha kwa walimu kwa kuwapatia zawadi ya shilingi milioni 1.2 pamoja na ahadi ya kuwapatia kompyuta kwa ajili ya kuongeza ari na morali wa kufundisha.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Elizabert Fabian, alisema kuwa shule ya Tumaini Junior imefanya mahafali mawili kwa mpigo mwaka huu, ambapo wanafunzi 78 wamehitimu elimu ya msingi na wanafunzi 14 wamehitimu elimu ya awali.

Sherehe hizo ziliambatana na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi pamoja na pongezi za wazazi na wadau wa elimu waliokuwepo kushuhudia mafanikio hayo.








Ends...

Post a Comment

0 Comments