Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua rasmi awamu ya tano ya kampeni yake maarufu ya Twenzetu Kileleni, ikilenga kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi kupitia Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika.
Katika uzinduzi huo, TANAPA imezitaja kampuni tatu zilizoidhinishwa kuratibu safari za kupandisha watalii kileleni kupitia njia tatu kuu za kupanda mlima huo ambazo ni Marangu, Machame na Lemosho.
Akiongea na waandishi wa habari mapema Agosti 29,2025 makao Makuu ya shirika hilo,jijini Arusha wakati akizindua kampeni hiyo,Naibu kamishna wa uhifadhi TANAPA, Missana Mwishawa alisema tukio hilo litakuwa ni kumbukumbu ya kitaifa na alama ya mshikamano wa Watanzania.
> “Kupandishwa kwa bendera ya Taifa kileleni siku ya Uhuru kutakuwa ni ishara ya uzalendo na fahari ya Watanzania wote. Ni tukio litakalobaki kwenye historia ya taifa letu,” alisema Mwishawa
Kwa upande wao, wawakilishi wa kampuni hizo tatu zilizopata kibali walielezea matumaini yao na dhamira ya kushirikiana na TANAPA kuhakikisha mafanikio ya kampeni hiyo.
Mwandishi wa kampuni ya Zara Tours Ltd, Faustine Chombo aliishukuru Tanapa kwa kuwaidhinisha kuratibu zoezi hilo kupotia njia Kongwe ya Marangu na wamejipanga kwa vifaa maalumu kwa watalii wakati wa kupanda mlima.Pia wageni watahudumiwa kwa chakula na maladhi pamoja na vifaa vya uokozi ikiwemo usafiri wa ndege.
> “Kampuni yetu inajivunia kuwa sehemu ya historia hii. Tunajipanga kutoa huduma za kitaalamu na salama kwa wageni wanaopanda mlima kupitia njia ya Marangu. Hii ni fursa ya kipekee ya kutangaza vivutio vyetu vya asili duniani.”
Naye mwakilishi wa kampuni ya African Scenic, Mery Njuguna aliishukuru Rais Samia Suluhu hasan kwa jitihada zake za kucheza filamu ya Royal Tour ambayo imeleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo kutokana na idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini kuongezeka.
> “Tumejipanga kuhakikisha kila mtalii atakayepanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia yetu anapata huduma za kiwango cha juu, usalama na kumbukumbu nzuri zitakazomfanya awe balozi wa utalii wa Tanzania duniani,” alisema.
Naye Experius Daniel mwongoza utalii wa kampuni ya utalii ya African Zoom Adventure, alibainisha kuwa njia ya Machame itakuwa kivutio kikubwa kwa wapenda changamoto na mandhari ya kipekee.
> “Tunataka kila mgeni ajisikie tofauti kupitia njia ya Lemosho. Hii kampeni ya Twenzetu Kileleni ni zaidi ya utalii, ni urithi wa taifa letu tunaouenzi na kuutangaza,” alisema.
Kwa upande wake afisa wa Uhifadhi wa hifadhi ya Raifa Kilimanjaro KINAPA,Vitus Mgaya alisema kuwa wao kama wenyeji wamejipanga vuzuri kuwapokea watalii wote wanaokuja na jupanda mlima kilimanjaro.
"Sisi kama KINAPA wenyeji wa kampeni ya Twendezetu Kileleni tunawahakikishia ulinzi na usalama idadi yoyote ya wageni watakao kuja kupanda mlima kilimanjaro katika kumbukizi ya miaka 64 ya uhuru"
Baadhi ya wadau wa utalii walioshiriki kwenye uzinduzi huo walipongeza TANAPA kwa ubunifu wa kampeni hiyo ambayo imekuwa na manufaa makubwa.
> “Kupandishwa kwa bendera siku ya Uhuru kutatufanya tuone fahari kubwa kama Watanzania. Vijana wetu pia watahamasika kupenda nchi yao na kushiriki katika uhifadhi.”
“TUPANDE PAMOJA KWA KESHO YETU, NA URITHI WETU.”
ends....
0 Comments