MIKOA ZAIDI YA 10 YAFUNIKA JOGGING YA TANZANIA SAMIA CONNECT ARUSHA,RC KIHONGOZI APONGEZWA ,TIZAMA PICHA UTAPENDA

WANANCHI WA ARUSHA WAJITOKEZA KWA WINGI KUSHIRIKI “JOGGING LA TANZANIA SAMIA CONNECT”

Na Joseph Ngilisho-ArushaDigital


Maelfu ya wakazi wa Jiji la Arusha na vitongoji vyake leo, Jumamosi Agosti 23, 2025, wamejitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Jogging na mazoezi ya viungo, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kilele cha Tamasha la Tanzania Samia Connect.


Tamasha hilo, ambalo limepambwa na shamrashamra mbalimbali, limekusudia kuadhimisha na kusherehekea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mbio za Jogging zilianza katika Uwanja wa Mgambo, eneo la Uzunguni jijini Arusha, ambapo mamia ya wananchi wa rika tofauti walishiriki kwa hamasa kubwa. Wengine walionekana wakiwa na mavazi ya michezo yenye nembo ya “Samia Connect”, huku nyuso za furaha zikigubika hafla hiyo ya kitaifa.


Mbali na michezo, wananchi pia waliendelea kunufaika na huduma mbalimbali zilizotolewa bure ikiwemo matibabu ya kitabibu, upimaji afya, utoaji wa vyeti vya kuzaliwa, pamoja na usajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Huduma hizo ziliwavutia wananchi wengi waliokuwa na changamoto ya kupata huduma hizo kwa urahisi.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Kenani Laban Kihongosi, ambaye ndiye muasisi na mratibu mkuu wa tamasha hilo, alibainisha kuwa lengo kubwa la Samia Connect ni kuwaleta wananchi pamoja kusherehekea mafanikio ya serikali na kuimarisha mshikamano wa kijamii.


“Tamasha hili ni sehemu ya kuthamini jitihada za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusukuma maendeleo ya Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla. Tunataka kila mwananchi ajihisi sehemu ya safari hii ya mafanikio,” alisema Mhe. Kihongosi.


Baadhi ya wananchi waliozungumza na vyombo vya habari walieleza kufurahishwa kwao na mbio hizo, wakisema zimekuwa ni fursa ya kuburudika, kushiriki katika michezo ya afya na kupata huduma muhimu bila gharama.


Tamasha la Tanzania Samia Connect linaendelea kufanyika jijini Arusha, likihusisha burudani mbalimbali, maonesho ya kazi za vijana na wanawake, pamoja na mijadala ya kimaendeleo inayolenga kumulika mafanikio ya serikali katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Baadhi ya mikoa iliyoshiriki Tanzania Samia connect Jogging ni pamoja Mkoa wa Dar es salaam,Arusha,Simiyu,Mara ,Manyara ,Kilimanjaro,Iringa,Dodoma,Geira na Kigoma.














Ends..

Post a Comment

0 Comments