ODERO ATOA WITO WA TAIFA KUINGIA KWENYE SAFARI YA UPONYAJI, ATOA TAFAKARI KWA VYAMA VYA SIASA

 Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


ARUSHA – Mwenyekiti wa Kamati ya Kusukuma Maridhiano Tanzania, Odero Odero, ameendelea kusisitiza umuhimu wa taifa kuingia kwa nguvu mpya katika hatua za maridhiano baada ya tukio la Oktoba 29, huku akizitaka pande zote za kisiasa kujifunza kutoka kwenye mifumo ya demokrasia iliyopevuka duniani.

Amesema kuwa wakati Tanzania inapitia kipindi chenye hisia tofauti na mitazamo inayogongana, ni wajibu wa viongozi na wananchi wote kuchagua njia ya hekima, utulivu na mazungumzo yanayojenga badala ya migawanyiko inayodhoofisha msingi wa taifa.

Katika salamu zake kwa Watanzania, Odero alikumbusha kuwa maridhiano si unyonge bali ni kifaa muhimu cha kuponya majeraha ya taifa—na ndiyo njia pekee ya kulinda amani ambayo imeitambulisha Tanzania kwa dunia nzima.

>

“Maridhiano si ishara ya udhaifu, ni uthubutu. Si kurudi nyuma, bali ni hatua ya kukomaa kisiasa na kijamii. Ni kujenga upya, sio kusahau,” alisema.


Akiwataja moja kwa moja wadau wakuu wa siasa nchini, Odero alivionya na kuvishauri vyama vikuu vya upinzani nchini hususani– CHADEMA na ACT-Wazalendo – kuiga mifumo ya mazungumzo na ustahimilivu ya mataifa yenye demokrasia ya muda mrefu kama Ulaya Magharibi na Marekani.

Amesema mataifa hayo, licha ya kuwa na tofauti kali za kisiasa, maamuzi magumu ya kiserikali na matamshi ya ukosoaji mkali, bado huwekeza nguvu kubwa katika kutafuta power of negotiations, power of dialogue, power of reconciliation na power of engagement.

>

“Pamoja na Marekani na Ulaya kutoa matamshi makali wanapoona kasoro za kidemokrasia, angalia jinsi wanavyotafuta kila fursa ya kuzungumza. Wanapishana kwa hoja, sio uhasama. Wanatofautiana kwa mawazo, sio kuvunja misingi ya pamoja,” alisema Odero , akisisitiza kuwa Tanzania nayo inaweza kufikia kiwango hicho kupitia misingi ya mazungumzo ya wazi na ya uwazi.


Odero  aliwataka Watanzania Kusikilizana kwa heshima bila kuhukumiana,Kuweka mbele nidhamu ya majadiliano kuliko hisia kali,Kushiriki kwa upana katika hatua za kitaifa za maridhiano.

Akihitimisha, alisisitiza kwamba Kamati ya Kusukuma Maridhiano itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya matumaini, ushirikiano na uzalendo uliopevuka.

>

“Tanzania yetu ni moja. Tuichague amani, tuichague maridhiano, tuijenge pamoja,” alihitimisha  Odero.


Ends..

Post a Comment

0 Comments