CCM YAKUSANYA BILIONI 86,GSM ACHANGIA BILIONI 10

 By Arushadigital -Dar es Salaam 


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekusanya Sh bilioni 86 katika uzinduzi wa harambee yake ya kutafuta fedha kwa ajili ya kukiwezesha chama kufanya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu.


Lengo la chama ni kukusanya Sh. bilioni 100 ambazo zitakiwezesha kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kujinadi kwa wananchi.


Kati ya fedha hizo zilizokusanywa katika uzinduzi wa harambee hiyo inayoendelea, fedha taslimu ni Sh. bilioni 56.31 na ahadi ni Sh. bilioni 30.2.


Katika harambee hiyo iliyofanyika leo Agosti 12,2025, Mlimani City, Dar es Salaam, kati ya fedha hizo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, amechangia Sh. milioni 100, huku Rais wa Zanzibar,  Dk. Hussein Ali Mwinyi, akitoa Sh. milioni 50.



Washiriki waliohudhuria harambee hiyo

Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia amewashukuru wote waliochangia chama na watakaoendelea kutoa michango yao kuwezesha kampeni za CCM.

“Kutoa ni moyo si utajiri, michango yenu itatuwezesha kufikia lengo na tutaweza kukamilisha kampeni zetu salama,” amesema.



Amehamasisha wote wanaotaka kukichangia chama wakiwamo, Diaspora wafanye hivyo kupitia utaratibu uliowekwa.


Katibu Mkuu CCM,  Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, awali amesema michango hiyo inaendelea mpaka Agosti 27, mwaka huu,  hivyo Watanzania wenye nia njema ya kuchangia wanaweza kufanya hivyo kwa ajili ya ujenzi wa nchi.

Post a Comment

0 Comments