WATU 25 WAFUKIWA NA KIFUSI KWENYE MGODI WA DHAHABU
By Arushadigital -SHINYANGA
Hali ya taharuki imetanda katika kijiji cha Nyandolwa Kata ya Mwenge mkoa wa Shinyanga baada ya ajali mbaya ya mgodi kusababisha watu 25 kufukiwa na kifusi cha udongo, kufuatia kuporomoka kwa sehemu ya mgodi wa dhahabu jana majira ya saa nane mchana.
Tukio hilo limetokea Agosti 12 majira ya saa 4 asubuhi wakati watu hao wakiendelea na shughuli za ukarabati wa maduara ya dhahabu.
Chifu Inspekta wa kikundi cha wachapakazi Gold Mine, Fikiri Mnwagi ambao ni wamiliki wa mgodi huo akizumgumza leo, amesema kuwa maduara hayo matatu yalikuwa katika ukarabati hali iliyopelekea ardhi ya eneo hilo kutitia na kufunika watu 25 ambao ni wafanyakazi na mafundi.
Amesema, baada ya kufunikiwa walikuwa wakifanya mawasiliano kati ya watu 6 ambao walikuwa katika duara namba 106 na wamefanikiwa kuwaokoa watu watatu huku bado shughuli za uokoaji zikiendelea.
"Duara namba 106 walikuwa watu 6 ambao tulifanikiwa kufanya mawasiliano nao kwa sauti ya mwangwi na kuokoa watu watatu, huku duara namba 20 na 103 hatujafanikiwa kufanya nao mawasiliano lakini juhudi Bado zinaendelea na tumechimba duara la ziada ili kuweza kuwafikia wengine pamoja na kupitisha maji na chakula" amesema Mnwagi.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro baada ya kufika eneo la tukio amewaomba wananchi wawe watulivu wakati zoezi la uokoaji bado linaendelea huku lengo kuu likiwa ni kuwaokoa watu wote na kufanya juhudi za kupata mawasiliano na wengine pia.
"Watu 25 walifukiwa na watatu tayari wameokolewa huku maduara mawili bado hatujafanyikiwa kupata mawasiliano nao lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha pia tunapata mawasiliano na kuwaokoa wote, duara namba 20 lina watu nane, duara namba 103 watu 11, na duara namba 106 watu sita na mpaka sasa tumeokoa watatu" amesema Mtatiro.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita,ametoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa eneo hilo na kuwataka waendelee kuwa watulivu wakati zoezi la uokoaji likiendelea.
"Watu wa mgodi huu wanaujirani mwema kwa sababu tangu tukio hili limetokea mafundi wa migodi jirani wameweka kambi eneo hili kuhakikisha zoezi zima la uokoaji linaenda vizuri nawashukuru sana kwa sababu waokoaji wa kwanza ni wakazi wa eneo husika" amesema Mhita.
Nao baadhi ya wakazi na wafanyakazi wa eneo hilo akiwemo Joseph Shahibu,wameishukuru serikali kwa juhudi zao za kuhakikisha watu wote waliofukiwa na Mgodi huo wanaokolewa huku wakiomba na wao wapewe nafasi ya kushiriki kuokoa wenzao.
Ends..
>
0 Comments