Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amefanya ziara ya kikazi katika Jiji la Arusha kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kisasa la Kituo cha Jiolojia Tanzania (TGC), mradi unaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 33.
Mradi huu unaojengwa kwa fedha za ndani ukiwa na lengo la kuongeza thamani ya madini ya vito yanayopatikana nchini.Jengo hilo linatarajiwa kukamilika baada ya siku 900.
Jengo hilo la ghorofa nane linajengwa katika eneo la kituo cha kuongeza thamani Madini(TGC )kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na Kituo hicho, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya Sita kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Mavunde alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za makusudi za kujenga miundombinu ya kisasa itakayowezesha vijana wa Kitanzania kupata ujuzi, ajira, na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.
>
“Kupitia mradi huu, tunataka kuhakikisha kuwa madini yote yanayochimbwa hapa nchini yanapata thamani zaidi kwa kuchakatwa na kutengenezwa hapa hapa nchini kabla ya kwenda kwenye masoko ya kimataifa,” alisema Mavunde.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya wazawa ya Skywards costraction Ltd na Lumocons Co. ltd ya jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa mhandisi msimamizi wa ujenzi huo, kupitia mkandarasi huyo,mradi umefikia zaidi ya asilimia 65 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Jengo hilo litakuwa na huduma za mafunzo ya uchakataji wa madini ya vito kama vile almasi, tanzanite na kinywe, pamoja na karakana za kisasa za kuongeza thamani ya madini hayo. Pia litakuwa kitovu cha utoaji wa huduma za kitalaam kwa wachimbaji, wafanyabiashara wa madini na wataalamu wa jiolojia.
Akizungumzia faida ya Mradi huo ni pamoja na kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wachakataji wa madini ya vito,Kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi,Kupanua wigo wa ajira na kuongeza kipato kwa Watanzania pamoja na kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa madini.
Wananchi wa mkoa wa Arusha pomoja na wadau wa sekta ya madini wameeleza matumaini yao juu ya mradi huo, wakisema utakuwa mkombozi kwa wachimbaji wadogo na vijana wanaotafuta ajira katika sekta hiyo.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuongeza thamani ya madini yetu. Hili jengo likikamilika, sisi wachimbaji tutafaidika zaidi,” alisema mmoja wa wachimbaji waliokuwepo katika eneo hilo.Alisema mmoja ya wadau wa Madini.
Awali Mkuu wa Mkoa Kenani Kihongosi aliishukuru serikali kupitia rais Samia Suluhu hasan kwa kuona umuhimu wa kuleta mradi huo wa ujenzi wa jengo ambapo pamoja na mambo mengine litachangia kuboresha mandhari ya jiji la Arusha na kuongeza uchumi katika mkoa huu.
Niishukuru sana serikali chini ya uongozi wa rais Samia kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni 30 kwa ujenzi wa kituo hiki cha uongezaji thamani ya madini ya vito na katika mkoa wetu jengo hili linakwenda kuongeza uchumi,kukuza biashara ya madini,kuongeza ajira na kukuza pato la Taifa"
Alisema ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi ya uchumi wa madini, kwa kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa kiwango kikubwa zaidi kupitia thamani inayoongezwa hapa nchini.
Msimamizi wa mradi huo ,Jumanne Shimba alisema kuwa mradi huo ulianza Agosti , mwaka 2024 kwa kubomoa jengo lililokuwepo na pindi litakapokamilika litakuwa na Kumbi za Mikutano na Maabara ya madini ya Vito kwa ajili ya kuwahudumia wadau wa madini.
Alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni kuondoa mabomba makubwa ya Maji yaliyobainika yapo ndani ya mradi huo na tayari taratibu za kuyaondoa zinaendelea ili kuruhusu mkandarasi kuendelea na shughuli za ujenzi.
Ends..
0 Comments