KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID IMELETA MAFANIKIO-MASWI

KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID YAZIDI KULETA MAFANIKIO, LAKINI VIJIJINI BADO KUNA PENGO

Na Joseph Ngilisho- Arusha

Kampeni ya kitaifa ya Mama Samia Legal Aid, iliyoanzishwa kwa lengo la kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wa kawaida, imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika maeneo mengi ya Tanzania, huku mamia ya wananchi wakiendelea kupata haki zao ambazo awali walizikosa kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya sheria na uwezo wa kifedha.


Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, kampeni hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi walio wengi, lakini bado kuna changamoto kubwa katika maeneo ya vijijini na baadhi ya miji midogo ambako huduma za msaada wa sheria hazijafika kikamilifu.


“Licha ya mafanikio tuliyoyapata, bado kuna maeneo mengi nchini ambako wananchi hawajui haki zao wala njia za kuzidai. Hili ni jambo linalohitaji nguvu zaidi, hasa kwa kushirikisha wadau wa sekta binafsi na mashirika ya kiraia,” alisema Maswi wakati wa kongamano la kitaifa la msaada wa sheria lililofanyika jijini Arusha.


Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais - Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Hanifa Ramadhan Said, alisema kampeni ya Mama Samia Legal Aid imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza imani ya wananchi kwa serikali, huku pia ikileta ushirikiano mpana kati ya wadau wa sekta ya sheria nchini.


“Tunaona kwa sasa wananchi wanakaribia zaidi serikali kwa sababu wanajua kuna masikio yanawasikia. Hii ni ishara nzuri ya utawala bora na uwajibikaji wa karibu na wananchi,” alisema Hanifa.


Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, aliwataka watoa huduma za msaada wa sheria kuongeza kasi, kutumia mbinu jumuishi na kuwa wabunifu zaidi ili kuhakikisha wananchi wote, hasa walioko maeneo ya pembezoni, wanapata huduma kwa wakati na kwa njia rafiki.


“Tunahitaji mawakili wa kujitolea, taasisi za kijamii na serikali za mitaa kushirikiana kwa karibu zaidi kuhakikisha mtu wa mwisho kabisa kijijini anapata msaada wa kisheria,” alisema Mwabukusi.


Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea kuungwa mkono na taasisi mbalimbali za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na vyama vya wanasheria nchini, ikiwa ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila ubaguzi wa kijamii au kijiografia.

Post a Comment

0 Comments