Mbunge wa Bukoba Mjini Wakili Steven Byabato aonya dhidi ya Siasa za Kuchafuana
Na Lydia Lugakila
Bukoba
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Wakili Steven Byabato, amewaomba wananchi wa Bukoba kutokubali kuyumbishwa na siasa za kuchafuana ambazo hazina msingi.
Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia siasa safi zenye kujenga na kukiheshimisha chama cha mapinduzi (CCM)
Byabato ametoa kauli hiyo julai 23, 2025
wakati wa hafla ya kukabidhi wakandarasi maeneo ya ujenzi wa miradi ya TACTIC kwa ufadhili wa benki ya dunia iliyofanyika eneo la soko kuu la Bukoba.
Byabato ameonyesha kusikitishwa na baadhi ya watu wanaochafua majina ya wengine kupitia siasa, huku akisisitiza kuwa wakati wote wa kipindi chake cha ubunge, amejitahidi kuendesha siasa ambazo hazina chuki wala uhasama.
Amezitaja juhudi zake za kuimarisha ushirikiano na jamii kama mojawapo ya mafanikio yake makubwa katika kipindi chake cha ubunge.
Akiwaeleza wananchi kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Byabato amewataka wote wanaotaka kugombea kufanya hivyo kwa kufuata maadili na bila kueneza chuki au fitina, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani iliyopo katika jamii.
Ameongeza kuwa ni Mungu pekee ndiye atakayekuwa na maamuzi sahihi katika uchaguzi huo.
“Katika uchaguzi wa mwaka 2020 tulikuwa na wagombea 57, lakini mwaka huu tumekuwa wagombea 14, hivyo Mungu ndiye atakayemchagua kiongozi sahihi,” alisema Mbunge Byabato, akihitimisha kwa maombi ya kupata uzima na mafanikio kwa awamu ijayo.
Aidha ametoa shukrani kwa Rais Samia pamoja na mkuu wa mkoa wa Kagera mhe, Hajjat Fatma Mwassa kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na uongozi mzuri huku akiwaomba wananchi kulinda vyema miradi inayotolewa na Serikali.
Hata hivyo amewashukuru viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Kagera kwa namna wanavyopambana na kihakikisha mkoa huo unakuwa na maendeleo.
0 Comments