By arushadigtal -Dodoma
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la mauaji ya raia mmoja, Frank Sanga (32), mkazi wa Kitongoji cha Mgomwa, Kata ya Matumbulu, Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, tukio hilo lilitokea Julai 19, 2025, majira ya saa 7:30 mchana, wakati marehemu akiwa amekamatwa kwa kosa la kuendesha pikipiki bila leseni, bila kuvaa kofia ngumu, na akiwa amebeba magunia matatu ya mkaa.
Frank alipelekwa kituo cha polisi, lakini alikataa kuendelea na safari ya kuelekea kituoni kabla ya ndugu zake kufika. Wakati hali hiyo ikiendelea, kundi kubwa la wananchi, wakiwemo ndugu wa Frank, walifika eneo hilo wakiwa na fimbo na silaha nyingine za jadi wakitaka kuchukua pikipiki yao kwa nguvu.
Katika hali ya taharuki, polisi mmoja anadaiwa kufyatua risasi ambazo zilimpiga Frank sehemu ya paja na nyonga. Alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma lakini alifariki dunia akiwa njiani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Agathon Hyera, amethibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi umeanzishwa mara moja ili kubaini ukweli wa tukio hilo na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuwa na makosa.
“Tunachunguza kwa kina. Kama itabainika kuwa askari alitumia nguvu kupita kiasi, hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa. Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mikononi,” alisema ACP Hyera.
Jeshi la Polisi limeendelea kuhimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya dola katika kuhakikisha usalama na utulivu vinadumishwa, hasa katika kipindi hiki ambacho matukio ya vurugu yanaripotiwa mara kwa mara kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi, huku familia na wananchi wa Matumbulu wakiendelea kusubiri matokeo rasmi ya uchunguzi huo.
Chanzo-Mwananchi
Ends ..
0 Comments