By arushadigtal-ARUSHA
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka nane, anayefahamika kwa jina la Karim Rahim, mwanafunzi wa darasa la pili, amefariki dunia katika mazingira yanayodaiwa kuwa ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya pazia, tukio lililotokea katika eneo la Osunyai Jr jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mwenyekiti wa mtaa huo, Silas Kimbei, tukio hilo limetokea nyumbani kwa bibi yake marehemu, ambako mtoto huyo alikuwa akiishi kwa muda. Mwenyekiti huyo amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa tayari Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha kifo hicho na mazingira yaliyopelekea tukio hilo la kusikitisha.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtoto huyo alipatikana akiwa amening’inia kwa kutumia kamba ya pazia, lakini kuna sintofahamu kubwa kutoka kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo ambao wameeleza mashaka yao kuhusu uwezo wa mtoto mdogo kama huyo kujinyonga kwa hiari. Baadhi yao wameomba uchunguzi wa kina kufanyika ili kubaini iwapo kuna mazingira ya uhalifu au hujuma katika tukio hilo.
“Hili ni jambo la kusikitisha sana. Tunaomba vyombo vya usalama vichunguze kwa undani. Hatuwezi kuamini kwa haraka kuwa mtoto mdogo wa miaka nane anaweza kujinyonga kwa fahamu zake mwenyewe,” alisema mmoja wa majirani ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Mpaka sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka kwa Jeshi la Polisi au mamlaka za afya kuhusu ripoti ya uchunguzi wa awali wa kifo hicho. Familia ya marehemu haijatoa tamko rasmi, huku jamii ikiendelea kutafakari kwa huzuni tukio hilo la kushtua.
Tunaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya uchunguzi huu.
Ends...
0 Comments