By Arushadigital-HANAN'G
MAHAKAMA ya Wilaya ya Hanan’g mkoani Manyara imewahukumu watu wawili kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani kila mmoja, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka kwa kundi bibi wa miaka 75 (jina limehifadhiwa).
Wawili hao, Nada Tluway (44), mkazi wa kijiji cha Meascon na Africanus Nicodemus (25), mkazi wa Katesh, pia wanatakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni moja kila mmoja kwa bibi huyo.
Akisoma hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Iloni Ponella, alisema mahakama imetoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 712 ya mwaka 2025, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na kosa la kubaka kwa kundi, kinyume cha Kifungu cha 131A (1) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Hakimu Ponella alisema washtakiwa walitenda kosa hilo Januari 2 mwaka huu katika kijiji cha Meascron.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo uliongozwa na mawakili wawili wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Ramadhan Mashauri na Maraba Masheku.
Washtakiwa walipopewa nafasi ya maombolezo, waliomba mahakama kuwapunguzia adhabu kwa kuwa wana wategemezi.
0 Comments