By Arushadigital
Kijana raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 17, Dunia Tuhenya, amepigwa risasi na kuuawa siku ya Ijumaa jioni katika jiji la Newburg, jimbo la New York, Marekani, tukio lililozua huzuni kubwa miongoni mwa jamii ya wenyeji na Watanzania waishio ughaibuni.
Kwa mujibu wa Polisi wa jiji hilo, tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya saa mbili usiku katika eneo la Chateau Village Kusini mwa jiji la Newburgh ambapo Dunia alipatikana akiwa na majeraha mabaya na alithibitishwa kufariki dunia papo hapo na wahudumu wa dharura.
Hadi kufikia Jumatatu asubuhi, hakuna mtu yeyote aliyekuwa amekamatwa na Polisi hawajatoa taarifa kuhusu watuhumiwa au sababu ya tukio hilo. Wananchi wametakiwa kujitokeza na kutoa taarifa yoyote itakayosaidia katika uchunguzi unaoendelea.
Tuhenya alikuwa mwanafunzi wa shule ya Newburgh Free Academy na alikuwa amemaliza mwaka wake wa tatu wa masomo. Marafiki na wanafunzi wenzake wamemuelezea kuwa alikuwa kijana “mtulivu, mchapakazi, na mwenye kupendwa na wengi,” huku akielezwa kuwa na ndoto za kuendelea na elimu ya juu.
Kifo cha Tuhenya ambaye alihamia Marekani pamoja na familia yake miaka michache iliyopita akitokea Tanzania kimegusa hisia za wengi, hasa miongoni mwa jamii ya Watanzania waishio Marekani, ambapo mamia walikusanyika kwa mkesha wa maombi na mshikamano uliowekwa maalum kwa ajili ya kumbukumbu yake mwishoni mwa wiki.
“Tumesikitishwa sana na kuondokewa na kijana mwenye ndoto na maisha mbele yake. Dunia alikuwa fahari ya familia na jamii. Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kuhakikisha haki inapatikana haraka.”— amesema Msemaji wa Jumuiya ya Watanzania New York.
0 Comments