Na Joseph Ngilisho-Arushadigital
MKUU wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi amefanikisha kukusanywa kiasi cha shilingi Milioni 418.4 huku fedha tasilimu ikiwa ni sh,milioni 1 katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Kuu la Christ Cathedral Church, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,
Harambee hiyo ilifanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC Jijini Arusha ambapo ,RC Kihongosi alimwakilisha Rais Samia Suluhu hasan aliyekuwa aongoze harambee hiyo.
Katika Hotuba yake, Kihongosi amesisitiza umuhimu wa kila mmoja kudumisha upendo, umoja na Mshikamano, akiwataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kujiepusha na vurugu wakati wa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
RC Kihongosi alilishukuru kanisa kwa kuendelea kusaidiana na serikali katika malezi ya watoto na jamii kwa ujumla na kubainisha kuwa kujengwa kwa kanisa hilo kutaimarisha zaidi imani na ukuaji wa kiroho kama hatua muhimu kwenye ujenzi wa maadili ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Ujenzi wa Jengo hilo unaotarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 3.8 za Kitanzania, ukiakisi matarajio ya Mpango kabambe wa Jiji la Arusha wa mwaka 2025, (Arusha 2025 Masterplan), ujenzi huo pia ukitajwa kutoathiri Jengo linalotumika sasa lililojengwa mwaka 1932, likihifadhi pia historia muhimu ya Tanzania kwa kipindi cha wakati wa Ukoloni. Harambee hiyo imeongozwa na maandiko matakatafu kutoka kwenye Kitabu cha Ezra 10.4 inayosema "Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe, uwe na moyo Mkuu ukaitende."
Waliohudhuria harambee hiyo ni pamoja na mhashamu Baba Askofu Dkt. Stanley Hotay, Askofu ya Dayosisi ya Mount Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo nchini, Viongozi mbalimbali wa dini pamoja na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM na Viongozi wa Serikali na Taasisi zake mbalimbali.
0 Comments