MISSENYI YASONGA MBELE DC MAIGA AONYESHA MWELEKEO WA MAENDELEO THABITI.
Na Lydia Lugakila-Misenyi.
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera, Mhe. Kanali Mstaafu Hamis Maiga, amesema kuwa wilaya hiyo imefanya maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali kutokana na ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Kanali Maiga ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwa waandishi wa habari waliotaka kujua masualabali mbali mbali ya ki maendeleo yanayoendelea kufanyika katika wilaya hiyo.
Maiga amesisitiza kuwa amani na usalama vilivyomo ni msingi wa mafanikio huku akifafanua kuwa Wilaya ya Missenyi imekuwa ikifanya kazi nzuri katika kutatua migogoro ya wakulima, wafugaji, na wafanyabiashara, hali inayochochea ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo.
Amesema kuwa ukusanyaji wa mapato umeongezeka kwa kiwango kikubwa, kutoka milioni 600 zilizokuwa zilikusanywa kwa mwezi miaka miwili iliyopita hadi shilingi bilioni 1.3 mwezi uliopita.
"Wenzetu TRA Mutukula upande wa Uganda ufanisi wao umekuwa mkubwa, kwa mwezi huu wameweza kupata makusanyo ya kiasi cha shilingi bilioni 8," alisema Kanali Maiga huku akionyesha pongezi kwa utendaji kazi mzuri wa ofisi hiyo"amesema kiongozi huyo.
Katika nyanja ya afya na Elimu, Maiga alikiri kuwa wilaya hiyo imeendelea kufanya vizuri, huku akisisitiza kuwa vijiji vyote 77 vimefikiwa na umeme, na maji na kwa mjini ni asilimia 98 na vijijini asilimia 74.
Vilevile, barabara nyingi za wilaya hiyo, ameongeza kuwa zinapitika kwa urahisi hata wakati wa mvua.
Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa mikutano ya ujirani mwema na raia wa Uganda imesaidia kuimarisha mahusiano ya kikazi, na hivyo kuondoa baadhi ya vikwazo vilivyokuwa vinakabili biashara kati ya Nchi hizo.
Kuhusu sekta ya kahawa, Maiga amesisitiza kuwa Wilaya ya Misenyi ni moja ya wazalishaji wakubwa wa kahawa huku akiweka wazi kwamba juhudi za serikali ya awamu ya sita zimeongeza bei ya zao hilo, hivyo kuwafanya wakulima wengi kuuza kahawa yao kwenye vyama vya ushirika.
"Kwa mwaka jana, kahawa ilikuwa ikiuzwa kwa zaidi ya shilingi elfu 5 kwa kilo, jambo lililowavutia wakulima,” amesema Maiga.
Kadhalika, Kanali Maiga ametangaza kuanzishwa kwa miradi saba ya kimkakati itakayogusa maendeleo ya wilaya hiyo, ikiwemo soko la kisasa linalotarajiwa kuanza kujengwa tarehe mosi mwezi Juni mwaka 2025, kwa gharama ya shilingi bilioni 9.
Ameongeza kuwa Majukumu mengine ni ujenzi wa soko la kimataifa la Kabakesa, upanuzi wa mwaro Kabindi, soko la ndizi Gera, na kuanzishwa kwa mnada wa ng’ombe Kakunyu.
Hata hivyo Mhe. Maiga ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa wilaya hiyo kipaumbele na kuleta miradi mikubwa yenye ubora inayosaidia kuboresha maisha ya wananchi, akiongeza kuwa maendeleo haya yameiimarisha imani ya wananchi kwa uongozi wa sasa.
0 Comments