Na Joseph Ngilisho -ARUSHA
KUNDI la watalii zaidi ya 130 kutoka nchini Uholanzi wametua Jijini Arusha na kutumia usafiri wa bajaj kutalii, kutoka jijini Arusha kuelekea uwanja wa ndege wa Kisongo ikiwa ni hatua ya ubunifu wa jeshi la polisi mkoani hapa kuhakikisha usafiri huo unakuwa na tija,salama na kivutio cha kukuza utalii mkoani hapa.
Akiongelea tukio hilo wakati watalii hao wakipanda Bajaji na kuongozwa na gari la polisi,mkuu wa polisi kikosi cha usalama barabarani mkoani Arusha (RTO),Zauda Mohamed alisema kikosi Chake kimelazimika kuwapatia mafunzo madereva wa bajaji jijini Arusha ili kuwajengea uwezo wa kusafirisha abiria kwa usalama hususani watalii ambao wanahitaji huduma nzuri ya usafiri wa Bajaj kuweza kujionea vivutio mbalimbali.
"Leo tupo hapa kutoa mafunzo kwa madereva wa pikipiki za magurudumu matatu(Bajaji)ili wajitambue kwa kutumia lugha nzuri kwa wateja ,pia tumewapatia elimu ya matumizi ya barabara na leo wanawabeba watalii kutoka katika hotel ya Gran Melia na Four Pont kwenda uwanja wa ndege wa Kisongo ikiwa ni hatua nzuri ya kuboresha usafiri huo"
Alisema watalii hao wamependa kutumia usafiri huo kwa sababu wanaweza kuyaangaza maeneo ya jiji hilo kwa ukaribu zaidi na kujionea manzari na vivutio mbalimbali.
Akiongea na waandishi wa habari mapema leo Jumanne Mei 27,2027 baada ya madereva hao kupatiwa mafunzo na kuwapeleka watalii 131 uwanja wa ndege kwa ajili ya kuelekea hifadhi ya Serengeti,mwongoza utalii wa kampuni ya utalii ya Tanzania Specialist ambayo ndio mwenyeji wa watalii hao,Nathan Maduga alisema tukio la kuwasafirisha watalii kwa kutumia Bajaji ni ubunifu wa kampuni hiyo na umekuwa kivutio kikubwa cha watalii pindi wanapo tua hapa nchini .
"Tupo hapa kushuhudia kitu cha tofauti ambapo kundi kubwa la watalii wanatumia usafiri wa Bajaj kuelekea uwanja wa ndege na hii ni ubunifu wa kampuni yetu kuhakikisha tunakuwa tofauti na wengije katika kukuza utalii "Alisema ,
Naye Mkurugezi wa kampuni ya utalii ya Tanzania Specialist,Epimark Mndevu alisema kampuni yake imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa taifa katika sekta ya utalii kuleta watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani kutoka na jitihada kubwa za kutangaza kampuni yake pamoja na vivutio vilivyopo hapa nchini.
"Wageni mnaowaona leo 131 ni sehemu ya idadi ndogo tu ya watalii tunaowapata kila mwaka na hii ni kutokana na matangazo yetu yanayoenda nchi nyingi duniani ,kampuni yetu inajitofautisha sana na kampuni nyingi za utalii nchini kutokana na uendeshaji wake"
Alisema tangu wameanzisha shughuli za utalii miaka nane iliyopita kampuni yake imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya utalii kwa kuleta idadi kubwa ya watalii na wamepanga kujikita pia kwenye utalii wa mambo ya asili ili kuchangia kwa kiasi kikubwa zaidi pato la taifa.
Ends...
0 Comments