DC LUGANGIRA APOKEA UJUMBE MZITO WA WABUNGE WA IPU ARUMERU ,AWAOMBA KUONGEZA WIGO WA MISAADA YA MIRADI
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
ARUMERU: Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amewataka washirika wa maendeleo kuongeza wigo wa miradi ya afya na kilimo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo, akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza matokeo ya maendeleo.
Lugangira alisema hayo jana wakati akipokea ujumbe wa wajumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), kutoka mataifa 16, waliotembelea miradi miwili ya maendeleo katika Wilaya hiyo, ikiwamo Zahanati ya Kiyoga na mradi wa umwagiliaji wa vijana katika Kijiji cha Oloigeruno, Arusha DC.
Alisema ziara hiyo imeonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha wananchi, hususani katika maeneo yenye mahitaji makubwa, wanapata huduma bora za afya na fursa za kiuchumi kupitia kilimo.
“Sisi kama Arumeru tupo tayari kuendeleza ushirikiano huu na mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, ikiwamo UNICEF, WHO na WFP, pamoja na Mastercard Foundation na TAHA,” alisema Lugangira.
Alisema ombi kubwa la Wilaya hiyo ni kuona miradi hiyo ikipanuliwa na kufika katika maeneo mengine ya Arusha DC, huku akisisitiza umuhimu wa kuifikisha pia Meru DC ili kuongeza wigo wa wananchi wanaonufaika.
“Kwa kuwa Wilaya yetu ina Halmashauri mbili, ni muhimu sana tufike pia Meru DC ili kuhakikisha tunachangia matokeo chanya na endelevu kwa wananchi wetu,” alisema.
TANZANIA YAPEWA HESHIMA
Kwa upande wake, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa, Hoyce Anderson Temu, alisema Tanzania imepata heshima kubwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa IPU, akitaka fursa hiyo itumike kufungua ushirikiano zaidi na mataifa mbalimbali duniani.
“Mkutano huu ni mlango wa kufungua ushirikiano na nchi mbalimbali duniani, hivyo naendelea kusisitiza usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali na wadau wengine,” alisema Temu.
Wajumbe hao walitembelea Wilaya ya Arumeru kujionea utekelezaji wa huduma za afya ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Kiyoga, pamoja na mradi wa vijana unaowawezesha kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa mbogamboga.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za Mkutano wa 153 wa IPU unaoendelea jijini Arusha, huku wajumbe kutoka mataifa mbalimbali wakipata fursa ya kutembelea maeneo ya Tanzania na kujionea maendeleo, utamaduni na urithi wa nchi.
Ends..











إرسال تعليق