Ad
Breaking🔥

KEMBAKI AWAASA WAHITIMU GHATI MEMORIALS MAARIFA NDIO UFUNGUO WA MAFANIKIO ,ASISITIZA GHATI 2027 KUHAMIA KIDIGIATAL WANAFUNZI KUTUMIA (TABLET) KISHKWAMBI

KEMBAKI AWAASA WAHITIMU GHATI MEMORIALS MAARIFA NDIO UFUNGUO WA MAFANIKIO ,ASISITIZA GHATI 2027 KUHAMIA KIDIGIATAL WANAFUNZI KUTUMIA (TABLET) KISHKWAMBI 

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


MKURUGENZI wa Shule za Ghati Memorial Tanzania na Nje ya Tanzania, Michael Mwita Kembaki, amesema elimu pekee haiwezi kuwa msingi wa mafanikio katika maisha, akisisitiza kuwa maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia ujuzi kutatua changamoto ndiyo msingi wa kumjenga kijana mwenye uwezo wa kukabiliana na dunia ya sasa.

                     
Kembaki alitoa kauli hiyo OKTOBA 4,2026 akiwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 13 ya kuhitimu elimu ya msingi, yaliyofanyika katika Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya Ghati Memorial, iliyopo Sinon jijini Arusha, ambapo jumla ya wanafunzi 141 wa Darasa la Saba walihitimu.


Akizungumza katika hafla hiyo, Kembaki alisema jamii imekuwa ikitumia kauli kwamba “elimu ni ufunguo wa maisha”, lakini kwa mtazamo wake, wanafunzi wanapaswa kwenda hatua zaidi kwa kutafuta maarifa yatakayowawezesha kutumia elimu waliyoipata katika kutatua changamoto za maisha.

“Elimu siyo ufunguo wa maisha. Maarifa ndiyo ufunguo wa maisha,” alisema Kembaki, huku akiwataka wahitimu hao kuendelea kujifunza, kuwa wabunifu na kutumia vipaji vyao katika kutatua changamoto zinazowazunguka.

Alisema shule hiyo inalenga kuwajenga wanafunzi kuwa viongozi wa kesho wenye uwezo wa kushindana, kubuni na kutumia maarifa yao kukabiliana na mahitaji ya dunia inayobadilika kwa kasi.

WAHITIMU WATAJA CHANGAMOTO

Awali, katika risala yao iliyosomwa na mhitimu Husna Hatibu, wahitimu hao waliushukuru uongozi wa Ghati Memorial kwa malezi na elimu waliyopatiwa, wakisema yamewasaidia kufanya vizuri katika masomo yao na kupata ufaulu wa Daraja A kila mwaka.

Hata hivyo, wahitimu hao walitaja baadhi ya changamoto walizoomba uongozi uzifanyie kazi, ikiwamo utoro unaochangiwa na baadhi ya wazazi kutolipa ada kwa wakati, hali ambayo, kwa mujibu wa risala hiyo, inaweza kuwaathiri wanafunzi katika mwendelezo wa masomo.

Pia waliomba shule iwe na uwanja wa michezo wa kutosha ili kuwawezesha wanafunzi kukuza vipaji vyao katika michezo mbalimbali sambamba na masomo.

Akijibu hoja hizo, Kembaki alisema uongozi tayari umeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto hizo, hasa suala la eneo la michezo na upanuzi wa shule.

Alisema shule imenunua eneo lililopo nyuma ya majengo yake na imeanza mchakato wa kupanua eneo la shule kwa kuwawezesha wakazi waliokuwa jirani na shule kuondoka kwa kuwapatia fidia, ili kupisha upanuzi wa eneo hilo.

“Tumeamua kuhakikisha shule hii inapata viwanja vya michezo vya kutosha. Tumenunua eneo lililopo nyuma ya majengo na tumeanza pia kuwahamisha majirani waliopo jirani na shule kwa kuwapatia fidia ili tupate eneo kubwa zaidi kwa ajili ya michezo mbalimbali,” alisema.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kukuza vipaji vyao nje ya darasa.

GHATI YAANZA KUHAMIA KIDIJITALI

Kembaki alisema shule hiyo pia imeanza kubadili mfumo wa ufundishaji kutoka ule wa zamani unaotegemea zaidi kukariri kwenda kwenye mfumo wa kisasa unaotumia teknolojia na ufundishaji wa vitendo.

Alisema walimu wameanza kupewa mafunzo ya matumizi ya kompyuta, huku shule ikiwa imenunua kompyuta na projekta kwa ajili ya kusaidia mchakato wa ufundishaji.

Alisema mpango huo utaendelea kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata vifaa vya kidijitali, ikiwamo tablets, zitakazotumika kuhifadhi vitabu na vifaa mbalimbali vya kujifunzia.

“Tunataka watoto wetu wawe na tablets kwa ajili ya kujifunza. Vitabu vinavyohitajika vitakuwa vimepakuliwa na kuhifadhiwa kwenye tablets zao ili mwanafunzi aweze kusoma kitabu anachohitaji popote alipo,” alisema.

Pia alisema shule inalenga kuimarisha huduma ya intaneti ili wanafunzi na walimu waweze kuitumia katika maeneo mbalimbali ya shule, hususan madarasani, kwa ajili ya kujifunza na kufundisha.

LIFE SKILLS KUPEWA KIPAUMBELE

Katika hatua nyingine, Kembaki alisema shule hiyo imepanga kuimarisha mafunzo ya ujuzi wa maisha (life skills) kwa wanafunzi ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.

Alisema mafunzo hayo yatawasaidia wanafunzi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi, kutumia vipaji vyao, kutatua changamoto na kujenga uwezo wa kujiajiri.

“Tunatambua kabisa tatizo la ajira katika nchi yetu, lakini pia ushindani uliopo katika soko la ajira duniani. Dhamira yetu ni kuwajenga vijana waweze kushindana katika soko la ajira, lakini si kwa ajira pekee; tunataka pia kuwajengea uwezo wa kujiajiri,” alisema.

Kembaki aliwapongeza wazazi kwa kutimiza wajibu wao wa kuwawezesha watoto kufikia hatua ya kuhitimu, huku akiwapongeza walimu kwa juhudi walizofanya kuhakikisha wanafunzi hao wanapata elimu, nidhamu na malezi yanayowaandaa kwa maisha ya baadaye.

Pia aliwapongeza wahitimu hao kwa kuvuka hatua hiyo, akisema wameonyesha juhudi katika masomo na mitihani mbalimbali waliyofanya kabla ya kufikia mahafali hayo.

Aliwataka wahitimu kutoridhika na ufaulu pekee, bali kuendelea kutafuta maarifa, kujiamini, kufanya kazi kwa bidii na kutumia vipaji vyao ili kuwa washindani na wabunifu katika maisha yao ya baadaye.

“Safari yenu haijaishia hapa. Mmehitimu elimu ya msingi, lakini maisha yanahitaji zaidi ya ufaulu. Tafuteni maarifa, tumieni vipaji vyenu na muwe tayari kujifunza kila siku huku mkiwaheshimu baba na Mama ndio mafanikio yenu,” alisema Kembaki.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post