Ad
Breaking🔥

ASKARI POLISI KARATU ATUHUMIWA KUMBAKA KINGONO MTOTO ANAYEMLEA,MKE ACHEKELEA

ASKARI ATUHUMIWA KWA TUHUMA ZA UKATILI WA KINGONO KWA MTOTO KARATU

.....Familia yamwomba Waziri Gwajima kutuma timu kuchunguza madai, yadai kesi ilifutwa baada ya shinikizo

Na Joseph Ngilisho | KARATU

ASKARI anayefanya kazi katika kitengo cha Ustawi wa Jamii Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, anadaiwa kuhusishwa na tuhuma za kumbaka na kumlazimisha kufanya vitendo vya kingono mtoto wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la tano.

Aidha familia ya mtoto huyo imemwomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, kuingilia kati na kutuma timu maalum kuchunguza suala hilo.

Kwa mujibu wa familia hiyo, mtoto huyo alitoa maelezo kuhusu tukio hilo na baadaye kupelekwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu, kabla ya taarifa hiyo kufikishwa katika Kituo cha Polisi Karatu Mjini ambako jalada la kesi lilifunguliwa.

Hata hivyo, familia inadai kuwa baadaye mama wa mtoto alishawishiwa na baadhi ya viongozi wa Polisi wilayani humo kuiondoa kesi hiyo ili kumlinda mume wake, anayedaiwa kuwa ni askari.

Familia hiyo inaeleza kuwa mama huyo alifikia hatua ya kusema amemsamehe mume wake na hivyo kuamua kufuta kesi, uamuzi ambao ndugu wengine wa mtoto wanasema hawakubaliani nao, wakisisitiza kuwa suala hilo linapaswa kuangaliwa zaidi kwa kuzingatia usalama na maslahi ya mtoto.

Kutokana na hali hiyo, familia imemuomba Waziri Gwajima kuingilia kati na kupeleka timu ya Wizara Karatu ili kufanya uchunguzi huru na wa kina kuhusu tuhuma hizo, ikiwemo madai ya mtoto, uchunguzi wa kitabibu, mwenendo wa jalada la kesi na mazingira yaliyopelekea kesi hiyo kuondolewa.

Familia hiyo pia imeeleza hofu kuhusu uwezekano wa suala hilo kuchunguzwa ndani ya mfumo wa Polisi wa eneo hilo pekee, kwa madai kuwa mtuhumiwa ni askari, hivyo kuomba mamlaka za juu kuhakikisha uchunguzi unafanyika bila mgongano wa maslahi.

Kwa msisitizo, familia inataka mamlaka zichunguze iwapo mtoto huyo alipata ulinzi na huduma stahiki baada ya kutoa madai hayo, pamoja na kubaini ukweli kuhusu mazingira ya kufutwa kwa kesi hiyo.

Wakati familia ikiendelea kuomba uchunguzi wa kina, Kusaga TV imefuatilia suala hilo kwa Jeshi la Polisi na imeelezwa kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na mamlaka husika.

Hadi sasa, tuhuma dhidi ya askari huyo bado zinahitaji uchunguzi na uthibitisho wa mamlaka za kisheria kabla ya kufikia hitimisho kuhusu hatia au kutokuwa na hatia.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post