Ad
Breaking🔥

DC LUGANGIRA AKABIDHIWA OFISI , AWEKA WAZI VIPAUMBELE VYA MAENDELEO ARUMERU,AHOJI MCHANGO WA WILAYA KUFIKIA UCHUMI WA DOLA TRIL 1.

LUGANGIRA AWEKA VIPAUMBELE VYA MAENDELEO ARUMERU

......Ahoji mchango wa wilaya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo 2050

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

Mkuu mpya wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, amesema ataelekeza nguvu katika kuboresha huduma za afya, elimu, kilimo, upatikanaji wa haki na mazingira ya uwekezaji ili kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo na kuchangia kufikiwa kwa uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.


Lugangira alisema hayo oktoba 9,2026 wakati akikabidhiwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa viongozi na watumishi wa umma kujiuliza namna wilaya hiyo itakavyotumia fursa zilizopo kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema Arumeru inapaswa kuweka mkazo katika mazao ya kimkakati kwa kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kupanua masoko ili bidhaa zinazozalishwa wilayani humo ziweze kushindana katika masoko ya kimataifa.


Katika sekta ya afya, alisema kipaumbele chake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, huku wagonjwa wakihudumiwa kwa wakati, kwa utu na malalamiko yao yakipatiwa ufumbuzi.

Alisema Arumeru inapaswa pia kujiandaa kuwa kitovu cha utalii wa kitabibu (medical tourism), akieleza kuwa azma hiyo haiwezi kufikiwa bila kuboresha huduma za afya na kukamilisha mahitaji muhimu ya utoaji wa huduma hizo.

Kuhusu elimu, alisema mafanikio hayapaswi kupimwa kwa ujenzi wa madarasa na majengo pekee, bali pia kwa ufaulu wa wanafunzi, mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

Alisema atafuatilia hali ya shule za wilaya hiyo ili kubaini zinazofanya vizuri na zile zenye changamoto, hatua itakayosaidia kuweka mikakati ya kuboresha matokeo ya elimu.

Katika upatikanaji wa haki, alisema atashirikiana na wabunge pamoja na mamlaka husika kutafuta namna ya kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi, ikiwamo kuimarisha upatikanaji wa huduma katika mahakama za mwanzo.

Kuhusu uwekezaji, Lugangira alisema anataka kuifanya Arumeru kuwa eneo linalovutia wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuweka mazingira rafiki, kupunguza urasimu na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Alisema uzoefu wa wawekezaji wanapopata huduma wilayani humo ni muhimu katika kujenga taswira ya Arumeru na kuamua iwapo wataendelea kuwekeza au kuhamasisha wengine kufanya hivyo.

“Natamani Arumeru iwe wilaya ambayo kila mwekezaji anayetaka kuwekeza atamani kufika hapa. Lazima tuhakikishe tunajipanga vizuri na kutoa huduma bora ili tuweze kuchangia katika kufikia maono ya Tanzania ya mwaka 2050,” alisema.

Ataka kusikiliza kero za wananchi

Katika kuimarisha uwajibikaji, Lugangira alisema ofisi yake itaweka utaratibu wa kusikiliza na kufuatilia utatuzi wa kero za wananchi kupitia njia tatu kuu ambazo ni ofisini, kwa kutembelea maeneo wanayoishi wananchi na kupitia mitandao ya kidijitali.

Alisema pia atatumia mfumo wa kufanya kazi kwa mzunguko, akitenga muda wa kukaa ofisini na kutembelea maeneo mbalimbali ya wilaya ili kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma, utekelezaji wa miradi na changamoto zinazowakabili wananchi.

Alisema lengo lake ni kufika katika kila kata ya Arumeru ili kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu mahitaji ya wananchi badala ya kutegemea taarifa za kwenye makaratasi pekee.

“Ndani ya miezi miwili hadi mitatu ya mwanzo kutakuwa na mchakamchaka wa kazi na ziara. Nataka ninaposimama kuzungumzia Arumeru, nisiizungumzie kwa kuisoma kwenye makaratasi, bali niwe nimefika katika kila kata na kuifahamu hali halisi ya wananchi,” alisema.

Alisema utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahitaji ushirikiano wa viongozi, watumishi wa umma, sekta binafsi na wananchi ili kuhakikisha fursa zilizopo Arumeru zinatumika kuongeza shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post