DC LUGANGIRA AWEKA MIKAKATI MITATU MIZITO YA MAENDELEO ARUMERU,KUANZA ZIARA KATA KWA KATA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ameweka mikakati mitatu ya kuongoza utekelezaji wa shughuli za maendeleo wilayani humo, akisisitiza ushirikiano kati ya Halmashauri za Meru na Arusha, uwajibikaji wa watumishi na kuimarisha huduma kwa wananchi.
Lugangira alisema mikakati hiyo inalenga kuitangaza Arumeru kimataifa, kuharakisha maendeleo ya wananchi na kuhakikisha viongozi wanatatua changamoto kwa kufika moja kwa moja katika maeneo yenye matatizo.
Alisema kaulimbiu ya kwanza ni “Arumeru Kimataifa”, akieleza kuwa wilaya hiyo ina fursa za uwekezaji, masoko na ushirikiano wa ndani na nje ya nchi ambazo zinapaswa kutumiwa kukuza uchumi.
Alisema pia anataka vivutio vya utalii vilivyopo Arumeru vitangazwe zaidi ili Watanzania na wageni wa nje wafahamu fursa zilizopo na kuvitembelea.
Kaulimbiu ya pili ni “Maendeleo ya Arumeru”, ambayo alisema inalenga kuhakikisha kila shughuli inayotekelezwa inazaa matokeo yanayoonekana kupitia huduma bora, ajira, ongezeko la kipato na kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema kwa kufanya hivyo, wilaya hiyo itachangia kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja.
Kaulimbiu ya tatu ni “Tukutane Sites”, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kufika katika maeneo ambayo miradi inatekelezwa au changamoto zinapotokea badala ya kutegemea taarifa za ofisini pekee.
“Kama kuna mradi, tukutane kwenye mradi. Kama kuna changamoto shuleni, tukutane shuleni; hospitalini, tukutane hospitalini; na kama kuna changamoto kijijini, tukutane kijijini,” alisema.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji, Lugangira alisema ataratibu vikao vya kukutana na watendaji wa Halmashauri za Meru na Arusha pamoja na viongozi wa taasisi zilizopo katika maeneo hayo.
Alisema pia atakutana na wenyeviti na watendaji wa vijiji, viongozi wa kata na tarafa, pamoja na mabaraza ya madiwani ya halmashauri hizo mbili, akibainisha kuwa ingawa zina mamlaka tofauti za kiutawala, zinapaswa kushirikiana kwa kuwa zinaunda wilaya moja.
Aidha, aliwataka wakuu wa idara na vitengo kuandaa taarifa fupi zinazoeleza mafanikio, changamoto, fursa na mapendekezo katika maeneo yao, akisema atafanya nao mazungumzo ya ana kwa ana ili kupata uelewa wa kina kuhusu mahitaji na namna ya kuboresha utendaji.
Alisema atafanya utaratibu kama huo kwa wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mkoa na wilaya ili kubaini maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu.
Kuhusu mawasiliano ya serikali, Lugangira aliagiza taarifa rasmi zinazotoka ofisini na kwenye mitandao ya kijamii ya halmashauri hizo kuhakikiwa ili kuhakikisha usahihi wake na kuendana na malengo ya maendeleo ya wilaya.
Alisisitiza kuwa anatarajia watumishi kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia matokeo, huku akipinga vitendo vya fitina na uchonganishi kazini.
“Sitaki fitina wala uchonganishi katika Wilaya ya Arumeru. Nataka tufanye kazi kwa ushirikiano na kila mmoja atamani kufanya kazi hapa kwa sababu ya fursa na matokeo tunayoyapata,” alisema.
Alisema kila mtumishi na kiongozi anapaswa kujiuliza kila siku mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa madaraka ni dhamana inayopaswa kuonekana kupitia huduma na maendeleo yanayowafikia wananchi.
“Kila mmoja wetu ajiulize: Leo nimefanya nini kubadilisha maisha ya mwananchi wa Arumeru? Hilo ndilo swali tunalopaswa kujiuliza kwa sababu dhamana tuliyopewa lazima ionekane katika maisha ya wananchi tunaowatumikia,” alisema.
Alisema yuko tayari kushirikiana na watumishi wote, kuwasikiliza na kuthamini ushauri wao, akisisitiza kuwa mafanikio ya Arumeru yanategemea mshikamano, nidhamu na dhamira ya pamoja ya kuleta maendeleo.
Ends


Post a Comment