Ad
Breaking🔥

CRDB YAKABIDHI VIFAA VYA OKSIJENI KCMC, KUIMARISHA HUDUMA ZA KUOKOA MAISHA

CRDB YAKABIDHI VIFAA VYA OKSIJENI KCMC, KUIMARISHA HUDUMA ZA KUOKOA MAISHA

..BENKI YAENDELEZA UWAKALA WAKE KWA JAMII, YASEMA UWEKEZAJI KATIKA AFYA NI SEHEMU YA KUJENGA JAMII YENYE USTAWI

Na Joseph Ngilisho | MOSHI

BENKI ya CRDB imezidi kuimarisha mchango wake katika sekta ya afya nchini baada ya kuikabidhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) vifaa saidizi vya utoaji wa oksijeni, vinavyolenga kuboresha huduma za matibabu na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo muhimu.

Msaada huo wa vifaa vinavyojulikana kama Oxygen Flow Meters umekabidhiwa Novemba 20, 2026, na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Cosmas Sadat, akishirikiana na Meneja wa Tawi la CRDB KCMC, Salestine Mchome.




Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Sadat alisema CRDB inatambua umuhimu wa sekta ya afya katika maendeleo ya jamii na kwamba mchango wa taasisi binafsi katika kuimarisha huduma za matibabu ni sehemu ya wajibu wake wa kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Alisema benki hiyo inaamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kutenganishwa na upatikanaji wa huduma bora za afya, hivyo itaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania.

Aliongeza kuwa msaada huo ni ishara ya dhamira ya CRDB ya kuendelea kushirikiana na taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa jamii, hususan hospitali zinazohudumia wagonjwa wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

"Kwetu CRDB, mafanikio ya benki hayaishii katika huduma za kifedha pekee, bali pia yanapimwa kwa mchango tunaoutoa katika kuboresha maisha ya jamii. Tunatambua umuhimu wa KCMC katika kutoa huduma za afya, ndiyo maana tumeona ni muhimu kuunga mkono juhudi zake kwa kuchangia vifaa vitakavyosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa," alisema Sadat.

Alisema CRDB itaendelea kutambua maeneo yenye mahitaji muhimu katika jamii na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mchango wa sekta binafsi unakuwa na matokeo chanya katika maisha ya wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Steven Kolimba, alisema vifaa hivyo vitasaidia kuboresha huduma za matibabu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa oksijeni kwa wagonjwa wanaohitaji.

Kolimba alisema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano wenye tija kati ya KCMC na CRDB, unaolenga kuimarisha uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma bora na kuokoa maisha ya wagonjwa.

"Tunawashukuru sana Benki ya CRDB kwa moyo wa kujitoa na kuunga mkono juhudi za hospitali yetu. Msaada huu ni ushahidi wa dhati wa ushirikiano wetu wenye lengo la kuokoa maisha na kuboresha afya za wagonjwa wetu. Mungu awabariki sana kwa kazi njema mnayoifanya kwa jamii," alisema Kolimba.

Alisema hospitali hiyo itaendelea kuthamini ushirikiano na wadau mbalimbali ambao wamekuwa sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya kwa jamii.

Hatua ya CRDB kuikabidhi KCMC vifaa hivyo inaendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya benki na taasisi za afya katika kuimarisha huduma za kijamii, huku ikisisitiza nafasi ya kampuni binafsi katika kuchangia maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post