Ad
Breaking🔥

MAKALLA: HORTILOGISTICA YAIFUNGULIA ARUSHA MILANGO YA UWEKEZAJI DUNIANI,AIPONGEZA TAHA KWA KUHESHIMISHA TAIFA


MAKALLA: HORTILOGISTICA YAIFUNGULIA ARUSHA MILANGO YA UWEKEZAJI DUNIANI

...Asema jukwaa hilo limeongeza hadhi ya Tanzania, kuchochea biashara na kuitangaza sekta ya mazao ya bustani kimataifa

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema jukwaa la kimataifa la HortiLogistica Africa 2026 limefungua milango mipya ya biashara na uwekezaji katika sekta ya mazao ya bustani, huku likiiweka Arusha katika nafasi muhimu ya kuunganisha wazalishaji wa Tanzania na masoko ya kimataifa.

Makalla alisema mafanikio ya jukwaa hilo ni ishara kuwa Arusha ina uwezo wa kuwa kitovu cha mikutano ya kimataifa ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuvutia wawekezaji na wanunuzi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Alitoa kauli hiyo baada ya kupokea ujumbe wa Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (TAHA), ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa chama hicho, Dkt. Jackline Mkindi, aliyefika ofisini kwake jijini Arusha Novemba 19, 2026, kumshukuru kwa mchango na ushirikiano wa Serikali ya Mkoa katika kufanikisha jukwaa hilo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema HortiLogistica Africa 2026 haikuwa maonesho ya kawaida, bali ilikuwa fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania, kuonesha uwezo wa sekta ya kilimo cha bustani na kuunganisha wadau wa ndani na wa kimataifa katika mnyororo mzima wa uzalishaji na biashara.

Alisema jukwaa hilo limechangia kuongeza mwonekano wa Arusha katika ramani ya kimataifa ya biashara, huku likifungua fursa kwa wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji kupanua shughuli zao na kupata masoko mapya.

HortiLogistica Africa 2026 lilifanyika Novemba 8 hadi 10 katika viwanja vya TGT Grounds, Wilaya ya Arumeru, likiwakutanisha wakulima, wazalishaji, wawekezaji, wanunuzi, wasafirishaji na wabunifu wa teknolojia kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Jukwaa hilo lililokuwa na lengo la kukuza biashara na uwekezaji katika mazao ya bustani, pia lilitoa fursa ya kuonesha teknolojia za kisasa zinazoweza kuongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa na ushindani wa mazao ya Afrika katika masoko ya kimataifa.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mkindi aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Arusha, Wizara ya Kilimo na taasisi nyingine za Serikali kwa ushirikiano na mchango wao katika maandalizi na utekelezaji wa jukwaa hilo.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kuandaa majukwaa makubwa yanayoweza kuleta matokeo ya kiuchumi na kufungua fursa kwa wadau wa sekta ya kilimo.

Mbali na manufaa kwa sekta ya kilimo, HortiLogistica Africa 2026 lilitarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi katika sekta nyingine ikiwemo hoteli, utalii, usafirishaji na huduma mbalimbali, hivyo kuongeza mzunguko wa fedha na fursa za biashara mkoani Arusha.

Jukwaa hilo liliandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na TAHA, likiwa sehemu ya jitihada za kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa ya mazao ya bustani.

Mafanikio ya tukio hilo yanaweka msingi wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuvutia mitaji, kupanua masoko na kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanapata nafasi kubwa zaidi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post