ROYAL GEMS YALENGA SOKO LA DUNIA KWA VITO VYA TANZANIA, YAZALISHA AJIRA KWA VIJANA ZAIDI YA 100
....Owais Hassan Yusuf asema Tanzania ina hazina kubwa ya vito, kampuni yawekeza katika ubunifu, uchakataji na utengenezaji wa mapambo ya kiwango cha kimataifa
Na Joseph Ngilisho | Dar es Salaam
WAKATI Tanzania ikiendelea kujijengea nafasi katika soko la kimataifa la madini ya vito, kampuni ya Royal Gems & Jewellery imeeleza mkakati wake wa kuongeza thamani ya rasilimali hizo kwa kuwekeza katika utengenezaji wa mapambo ya dhahabu, almasi na vito mbalimbali, hatua inayolenga kukuza biashara, kutoa ajira na kuwajengea vijana ujuzi wa kitaalamu.
Akizungumza katika Mkutano wa Wawekezaji wa Madini na Usiku wa Madini uliofanyika jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara wa kampuni ya Royal Gems & Jewellery, Owais Hassan Yusuf, alisema Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini ya vito yanayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Tanzanite kutoka Mererani, madini ya vito kutoka Mahenge na Tunduru, hivyo kuna fursa kubwa ya kukuza uchumi kupitia uchakataji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na madini hayo.
Alisema kampuni hiyo imejikita zaidi katika biashara ya vito vya thamani na utengenezaji wa mapambo badala ya uchimbaji, ikiwa na karakana inayotumia ujuzi wa mafundi wazawa kutengeneza bidhaa mbalimbali kulingana na mahitaji ya wateja.
"Hatuchimbi madini, lakini tunajihusisha na biashara ya dhahabu na vito vya thamani pamoja na kuvitengeneza. Tunataka kuonesha namna tunavyoweza kuongeza thamani ya madini yanayotoka Tanzania kwa kuyabadilisha kuwa bidhaa zenye ubora na mvuto katika soko," alisema Yusuf.
Alisema moja ya maeneo ambayo kampuni hiyo imewekeza ni ubunifu wa mapambo maalumu, ambapo wateja wanaweza kuwasilisha michoro au aina ya bidhaa wanayotaka na mafundi wa kampuni hiyo kuitengeneza kulingana na maelekezo yao.
Alisema uwezo huo wa kutengeneza mapambo kwa kuzingatia mahitaji binafsi ya wateja ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kushindana katika soko la kimataifa.
"Unaweza kuja na design yako, hata kama umeichora kwenye kitabu, tunaweza kuitengeneza. Tuna mafundi wenye ujuzi mkubwa na tunaamini kazi wanazofanya zinaweza kukidhi viwango vinavyohitajika katika soko la kimataifa," alisema.
AJIRA KWA VIJANA ZAIDI YA 100
Katika hatua nyingine, Yusuf alisema kampuni hiyo imekuwa ikichangia katika kukuza ajira kwa Watanzania, hususan vijana na wanawake, kupitia shughuli za utengenezaji wa vito pamoja na kuwapatia mafunzo ya vitendo wanaotaka kuingia katika taaluma hiyo.
Alisema zaidi ya vijana na wanawake 100 wamepata fursa za ajira na kujifunza ujuzi mbalimbali kupitia shughuli za kampuni hiyo, ikiwemo kuwapa nafasi wanafunzi na vijana wanaohitaji uzoefu wa kazi kupitia programu za mafunzo kwa vitendo.
Alisema uwekezaji katika kuwajengea uwezo mafundi wazawa ni muhimu kwa sababu unasaidia Tanzania kuwa na wataalamu wanaoweza kushughulikia hatua mbalimbali za utengenezaji wa vito badala ya kutegemea utaalamu kutoka nje ya nchi.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendesha takribani maduka 15 kupitia chapa mbalimbali za biashara, ikiwemo Royal, Queens, Exotic, The Capital, Zench Treasure na Gems of Tanzania.
ZAIDI YA MIAKA 20 KATIKA BIASHARA YA MADINI
Akizungumzia uzoefu wa kampuni hiyo, Yusuf alisema familia yao imekuwa katika biashara ya madini na vito vya thamani kwa zaidi ya miaka 20 nchini Tanzania, huku historia ya shughuli hizo katika familia ikifikia zaidi ya vizazi 12.
Alisema kampuni hiyo imeendelea kupanua wigo wa biashara kwa kuzingatia tofauti za masoko na mahitaji ya wateja katika maeneo mbalimbali nchini.
Alitaja maeneo ambayo biashara zao zinapatikana kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Arusha na Mwanza, huku kila soko likiwa na chapa inayolenga kukidhi mahitaji ya wateja wake.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kukuza biashara ya vito vya thamani nchini na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana Tanzania zinanufaisha zaidi uchumi kupitia biashara, ubunifu, ajira na uongezaji thamani.
Yusuf alisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya madini katika kuitangaza Tanzanite na vito vingine vya Tanzania, huku ikilenga kuimarisha nafasi ya bidhaa zinazotengenezwa nchini katika masoko ya ndani na kimataifa.
Ends

Post a Comment