AIRTEL AFRICA YAENDELEA KUWA KINARA KATIKA UWEKEZAJI
Na Joseph Ngilisho|ArushaDigital| DUBAI
KAMPUNI ya Airtel Africa itaendelea kuwa kinara katika uwekezaji wa miundombinu, teknolojia na ubunifu, ikiwa na lengo la kuboresha huduma kwa wateja wake milioni 183.5 barani Afrika na kuongeza wigo wa ujumuishaji wa kidijitali na kifedha.
Akizungumza mwanzoni mwa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema kampuni hiyo itaendelea kuweka mteja katikati ya uwekezaji na ubunifu wake kwa kusikiliza mahitaji yao na kuboresha huduma.
“Kaulimbiu ya mwaka huu, ‘The Extra Mile’ (Kwenda Hatua ya Ziada), inaendana na dhamira yetu ya dhati ya kuwathamini wateja wetu. Tunafanya hivyo kwa kuboresha jinsi tunavyowahudumia, kusikiliza na kujifunza kutoka kwao, na kuchukua hatua madhubuti zinazolingana na mahitaji na matarajio yao,” alisema.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Airtel Africa imeongeza zaidi ya tovuti 3,250 za mawasiliano na kilomita 3,200 za mkongo wa fibre, huku ikiendelea kuwekeza katika maduka na njia nyingine za usambazaji.
Taldar alisema kampuni hiyo pia imeongeza matumizi ya Akili Bandia (AI) katika kuboresha huduma za kidijitali, huku ikizindua huduma ya Spam Alert, inayojulikana kama “Kataa Matapeli”, kwa ajili ya kuwakinga wateja dhidi ya jumbe za utapeli na matangazo yasiyotakiwa.
Aidha, alisema Airtel imeanza kibiashara huduma ya satelaiti ya Direct-to-Device (D2D) inayolenga kuwaunganisha wateja katika maeneo ya vijijini ambayo hayajafikiwa na mtandao au yanayopata huduma duni.
Kwa mujibu wa Taldar, huduma hiyo inawawezesha wateja wenye simu janja zinazooana na teknolojia hiyo kuendelea kuwasiliana hata katika maeneo yasiyofikiwa na minara ya kawaida ya mawasiliano.
Alisema katika kuimarisha zaidi huduma kwa wateja, timu ya Airtel itatembelea masoko 14 ili kukutana nao, kusikiliza maoni yao na kubuni mbinu mpya za kuongeza ubora na uaminifu wa huduma.
MWISHO



إرسال تعليق