SHOMARI ATEMA NYONGO KALI MIKOPO YA ASILIMIA 10 ,ISIWE CHANZO CHA WANAWAKE KUKATA TAMAA,ATAKA SUALA LA KISINGIZIO CHA MIFUMO LIKOME,JIJI LA ARUSHA ALIPONGEZA KWA KUKOPESHA
Aagiza halmashauri ziondoe vikwazo vya mifumo, Arusha kutenga Sh7.8 bilioni kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Zainab Shomari, amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinaondoa vikwazo vya kiutendaji vinavyowafanya baadhi ya wanawake kushindwa kunufaika na mikopo ya asilimia 10, akisema mpango huo haupaswi kuwa chanzo cha kukatisha tamaa wananchi.
Shomari amesema licha ya Serikali kuweka mfumo huo kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi, bado baadhi ya walengwa wamekuwa wakikwama kutokana na changamoto za mifumo na taratibu ndefu za upatikanaji wa fedha hizo.
Akizungumza wakati wa ziara yake Mkoa wa Arusha Agosti 6,2026 , Shomari alisema amebaini uwepo wa waombaji ambao waliingia kwenye mfumo wa mikopo lakini hawakufanikiwa kupata fedha kutokana na changamoto za kiutendaji.
“Nimepata taarifa nyingi kuhusu changamoto ya mfumo. Kuna watu waliingia kwenye mfumo kipindi kilichopita, lakini baada ya mchakato kusitishwa wakabaki wanaonekana kwenye mfumo bila kupata mkopo. Hawa ni lazima tuwasaidie kutatua changamoto zao ili wanufaike,” alisema.
Aliagiza halmashauri kushirikiana na viongozi wa maeneo husika kubaini waombaji wenye changamoto hizo na kuwapatia suluhisho badala ya kuendelea kuzungushwa katika taratibu zisizo na mwisho.
“Safari ya kupata mkopo isiwe safari ya kwenda na kurudi kila siku mpaka mtu anavunjika moyo. Tufanye mchakato huu uwe wenye matokeo na fedha ziwafikie walengwa,” alisema.
Shomari alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata mitaji ya kuendesha shughuli za kiuchumi, ndiyo maana mpango huo umeendelea kuboreshwa kutoka asilimia 10 kuelekea asilimia 15 kutokana na mahitaji yanayoongezeka.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ametangaza mpango wa kutoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Sh bilioni 7.8 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kayombo, amesema fedha hizo zitatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na marejesho ya mikopo iliyotolewa awali.
Kayombo amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, halmashauri hiyo imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 13.9 kwa makundi hayo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Jiji la Arusha lilikusanya Sh bilioni 35.7 za mapato ya ndani na kutenga fedha za mikopo hiyo kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
Katika kipindi hicho, Sh bilioni 3.4 zilitolewa kwa vikundi 272, ambapo wanawake walipokea Sh bilioni 2.4 kupitia vikundi 194, vijana walipata Sh milioni 888.8, huku watu wenye ulemavu wakipokea Sh milioni 177.9.
Kwa mwaka mpya wa fedha, Kayombo alisema wanawake watanufaika na Sh bilioni 3.1, vijana Sh bilioni 3.1 na watu wenye ulemavu Sh bilioni 1.5.
Hata hivyo, amebainisha kuwa changamoto ya marejesho bado ipo, ambapo tangu mwaka 2016/2017 hadi 2025/2026, halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 34.4, huku Sh bilioni 21.5 pekee zikiwa zimerejeshwa.
Alisema deni linalosubiri marejesho ni Sh bilioni 15.9, huku hatua za kisheria zikianza kuchukuliwa kwa wale waliomaliza muda wa mikataba bila kurejesha fedha hizo.
Katika ziara hiyo, Shomari pia aliwapongeza viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha kwa kazi waliyoifanya katika kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi.
Alisema UWT Taifa imeanza ziara katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuwashukuru wanawake na viongozi waliojituma katika kukijenga chama na kuwafikia wananchi.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Arusha, Mary Kisaka, alisema ziara ya Shomari imeongeza hamasa kwa wanawake na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya kiuchumi.
Kisaka alisema Mama Shomari ametembelea miradi mbalimbali ya wanawake ikiwemo uzalishaji wa bidhaa za usafi, ufugaji wa kuku na uzalishaji wa mayai, huku akitoa maelekezo ya namna ya kuiongezea tija.
“Umetufanyia kazi kubwa. Umetembelea miradi ya wanawake na kutoa maelekezo muhimu ya kuongeza nguvu kwenye shughuli wanazofanya. Tunakushukuru kwa kututia moyo,” alisema Kisaka.
Aliomba salamu zifikishwe kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia amani na maendeleo nchini.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Arusha, Flora Zelothe, alisema wanawake wa mkoa huo wameendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Zelothe alisema Arusha imeongoza kitaifa kwa kuchangia zaidi ya Sh milioni 52 katika kampeni ya Ukoa Maisha Gala, huku Wilaya ya Arusha ikichangia Sh milioni 11.
Hata hivyo, aliomba Serikali kupitia taasisi za fedha kurahisisha masharti ya mikopo ya Mfuko wa Mama Samia ili wanawake wengi zaidi wajasiriamali waweze kunufaika.
Alilipongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuwashirikisha UWT katika usimamizi wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10, akizitaka halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
MWISHO












إرسال تعليق