Na Mwandishi wa A24tv .
Wananchi Waaswa Kujifunza Zaidi Kuhusu Kahawa katika Maonesho ya Nane Nane
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Fatma Almasi Nyangasa amewaasa Wananchi wanaotembelea Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayofanyika kwenye viwanja Vya Dkt John S Malecela kutumia fursa hiyo kujifunza kuhusu thamani ya mazao mbalimbali, hususan kahawa, badala ya kutembelea mabanda kwa lengo la kutazama pekee.
Nyangasa amayasema hayo leo August 6,2026,alivotembelea banda la Bodi ya Kahawa Tanzania, amesema ametoka na maarifa mapya kuhusu matumizi mbalimbali ya kahawa ambayo wengi hawajawahi kuyafahamu.
Amesema mbali na kutumika kama kinywaji, kahawa ina matumizi mengine mengi ikiwemo kutengeneza bidhaa za urembo kama coffee scrub, ambapo machicha yanayobaki baada ya kutengeneza kahawa hutumika kama malighafi ya bidhaa hizo.
Aidha, ameongeza kuwa wataalamu wa Bodi ya Kahawa wamekuwa wakitoa elimu kuhusu namna sahihi ya kuandaa kahawa, wakieleza kuwa kahawa haipaswi kuchemshwa, kwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri ubora wake, Badala yake, wananchi wanafundishwa njia sahihi za kuiandaa ili kuhifadhi ladha na virutubisho vyake.
Elimu hiyo pia inahusisha kiwango kinachofaa cha matumizi ya kahawa, muda unaofaa wa kuitumia pamoja na faida zake kiafya inaponywewa kwa usahihi.
Nyangasa amesema ujio wake katika banda la Bodi ya Kahawa umemwezesha kupata maarifa ambayo yatamsaidia kutumia kahawa kwa njia bora zaidi, huku akiwahimiza Watanzania wengine kutembelea banda hilo ili kujifunza kuhusu aina mbalimbali za kahawa zinazozalishwa nchini pamoja na fursa zinazotokana na zao hilo.
Amesisitiza kuwa maonesho ya Nane nane ni jukwaa muhimu la kujifunza teknolojia, ubunifu na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, hivyo wananchi wanapaswa kuyatumia kama nafasi ya kupata elimu itakayowasaidia kuboresha afya, biashara na maisha yao kwa ujumla.
Mwisho.

إرسال تعليق