LUKUMAY AMPONGEZA RAIS SAMIA, MSUMI KWA UWEKEZAJI KITUO CHA AFYA NDURUMA
....Asema huduma za upasuaji wa dharura na vifaa tiba zimeimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Arumeru Magharibi
Na Joseph Ngilisho, ARUMERU
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumay, amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, akisema ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya umeongeza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Dkt Lukumay alitoa kauli hiyo leo Septemba 17,2026 wakati wa ziara yake ya kutembelea, kukagua na kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Nduruma, wilayani Arumeru, ambapo alitembelea Kituo cha Afya Nduruma na kujionea huduma zinazotolewa, ikiwamo upasuaji wa dharura kwa akina mama.Mbunge huyo alisema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya afya unaendana na msisitizo wa Rais Samia katika kuimarisha huduma za afya kinga na tiba, huku akieleza kuridhishwa na maendeleo ya Kituo cha Afya Nduruma.
“Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele kwenye afya kinga. Tangu Serikali iingie madarakani, tumeshajenga hospitali za wilaya 119, vituo vya afya 179 na zahanati 700,” alisema.
NDURUMA YAGEUKA KITUO CHA RUFAA
Alisema huduma hizo ni sehemu ya uwekezaji unaosaidia wananchi kupata matibabu karibu na maeneo yao ya makazi, badala ya kutegemea hospitali za rufaa kwa kila tatizo la kiafya.
Akizungumzia huduma za afya ya mama na mtoto, mbunge huyo alisema kituo hicho kina wodi ya wazazi na vifaa vya kusaidia huduma za uzazi, huku akipongeza uwepo wa madaktari wenye uwezo wa kufanya upasuaji wa dharura wa kujifungua.“Kilichonifurahisha zaidi ni kuona kituo hiki kina uwezo wa kutoa huduma ya msingi ya upasuaji wa dharura. Hapa wana madaktari waliobobea, wanafanya upasuaji wa kuokoa maisha ya akina mama,” alisema.
Aliongeza kuwa Kituo cha Afya Nduruma kinahudumia zaidi ya zahanati tisa, hivyo kuwa na nafasi muhimu katika mfumo wa rufaa kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya kutoka maeneo jirani.
AMpongeza MSUMI
Dkt Lukumay pia alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Suleman Msumi, kwa juhudi za kuimarisha huduma za afya katika halmashauri hiyo, akisema ufuatiliaji wa mahitaji ya vituo vya afya na matumizi ya mapato ya ndani katika ukarabati ni hatua zinazosaidia kuboresha mazingira ya kutolea huduma.
“Nimshukuru mkurugenzi kwa kazi anayofanya kuhakikisha kwamba mahitaji ya kituo kama hiki yanapatikana. Vile vichache ambavyo havipo, vinavyohitaji ukarabati, vifanyiwe ukarabati,” alisema.
Alisema baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya zinahitaji ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa wananchi, watumishi wa afya na wadau wengine ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.
WITO KWA WANANCHI
Mbunge huyo aliwataka wananchi wa Nduruma kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutunza miundombinu ya afya na kutumia huduma zinazotolewa katika kituo hicho.
Alisema watumishi wa afya wanaendelea kufanya kazi kwa kujituma, licha ya changamoto za mazingira ya kazi, na kuwataka wananchi kuwaunga mkono katika juhudi za kuboresha afya za jamii.
Dkt Lukumay alisisitiza kuwa uwekezaji katika vituo vya afya ni muhimu katika kupunguza umbali wa wananchi kufuata huduma, hasa huduma za uzazi na matibabu ya dharura.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya shughuli za Mbunge wa Arumeru Magharibi za kutembelea maeneo mbalimbali ya jimbo, kukagua utekelezaji wa huduma na kusikiliza kero za wananchi kwa lengo la kuzifikisha kwenye mamlaka husika.
Ends


Post a Comment