Breaking🔥

MAKALLA ATOA ONYO: MSITUMIE KISINGIZIO CHA TAKUKURU KUCHELEWESHA MIRADI,TAKUKURU YAFICHUA KERO ZINAZOKWAMISHA MIRADI ARUSHA

MAKALLA: RUSHWA SI JUKUMU LA TAKUKURU PEKE YAKE

...Asema fedha za wananchi zisichepushwe, TAKUKURU isitumike kama kisingizio cha kuchelewesha miradi

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kuachiwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pekee, akitaka viongozi, watendaji wa Serikali, taasisi za umma na wananchi wote kuwajibika katika kulinda fedha na rasilimali za umma.

Makalla amesema bila ushirikiano wa wadau wote, juhudi za Serikali katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa zinaweza kukabiliwa na changamoto, ikiwamo ucheleweshaji wa miradi, upotevu wa rasilimali na wananchi kukosa huduma kwa wakati.

Alitoa kauli hiyo jana, Agosti 10, 2026, wakati akifungua warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo Mkoa wa Arusha, iliyowakutanisha viongozi na watendaji wa Serikali, halmashauri, taasisi za udhibiti, vyombo vya sheria na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Makalla alisema mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji mfumo shirikishi unaohusisha Serikali, vyombo vya sheria, taasisi za udhibiti, viongozi wa dini na jamii, kwa kuwa kila upande una wajibu wa kulinda misingi ya haki, uadilifu, usalama na utawala bora.

Alisema mahakama, polisi, taasisi za dini na TAKUKURU ni sehemu muhimu ya mfumo wa usimamizi wa nchi na kwamba endapo kila taasisi itashindwa kutekeleza wajibu wake, misingi ya utawala bora na uwajibikaji inaweza kudhoofika.

“Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu. Tutimize wajibu wetu,” alisema Makalla.

Katika hatua nyingine, Makalla aliwataka watendaji wa Serikali kutotumia ufuatiliaji wa TAKUKURU kama sababu ya kusimamisha au kuchelewesha miradi ya maendeleo, akisema kazi ya taasisi hiyo ni kulinda fedha za wananchi na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa usahihi.

“Tusitumie TAKUKURU kama chaka la kuchelewesha miradi. TAKUKURU inapofuatilia mradi, lengo ni kuhakikisha mambo yanaenda vizuri na hakuna fedha za wananchi zinazopotea,” alisema.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za udhibiti ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotengwa.

Kwa mujibu wa Makalla, ufuatiliaji wa TAKUKURU unapaswa kuchukuliwa kama sehemu ya juhudi za kulinda rasilimali za umma na si kikwazo cha utekelezaji wa miradi.

Aonya kuchepusha fedha

Makalla pia alisisitiza kuwa fedha zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kufika katika maeneo yaliyokusudiwa na kutumika kwa kazi zilizoainishwa, akionya dhidi ya vitendo vya kuzichepusha.

Alisema mabilioni ya fedha yanayotengwa kupitia bajeti za Serikali yanapaswa kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi, hivyo viongozi na watendaji wanaosimamia fedha hizo wanapaswa kuwa waaminifu, kuzingatia sheria na kutanguliza maslahi ya umma.

“Fedha nyingi zinazotolewa na Serikali na kutajwa katika bajeti zinapaswa kufika mkoani na kutumika kwa kazi iliyokusudiwa. Hakuna kutengeneza namna yoyote ya kuzichepusha. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeweka msingi mzuri wa maendeleo,” alisema.

Alisema uadilifu katika usimamizi wa fedha za umma unapaswa kwenda sambamba na hofu ya Mungu, uzingatiaji wa sheria na utendaji wa haki.

Makalla pia aliwataka watendaji wanaohusika na ukaguzi, ufuatiliaji na usimamizi wa fedha za umma kulinda uhuru wao wa kitaaluma na kuepuka mazingira yanayoweza kuathiri uadilifu wao.

Aliwataka kuepuka kupokea zawadi, huduma au upendeleo kutoka kwa watu wanaowasimamia au kuwafanyia ukaguzi, akisema vitendo hivyo vinaweza kuathiri uwezo wao wa kufanya maamuzi kwa uhuru na haki.

Aataka taarifa za miradi kwa wakati

Makalla alisema Serikali inahitaji taarifa sahihi na za wakati kuhusu utekelezaji wa miradi ili viongozi waweze kutambua changamoto mapema, kupima hatua zilizofikiwa na kuchukua hatua kabla matatizo hayajawa makubwa.

Alisema utafiti, uchunguzi, ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ni muhimu kwa kuwa taarifa zinazopatikana kutoka kwa taasisi husika zinaisaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi.

“Changamoto za miradi zinapaswa kubainika mapema na kushughulikiwa kabla hazijasababisha hasara kwa Serikali na wananchi,” alisema.

Nguvilla: Utawala bora ni lazima


Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvilla, alisema viongozi mkoani humo wana wajibu wa kuimarisha utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Nguvilla alisema mapambano dhidi ya rushwa katika utekelezaji wa miradi yanapaswa kupewa kipaumbele, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama katika Mkoa wa Arusha.

Alisema viongozi wanapaswa kuhakikisha maelekezo yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi, huku wakisimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Miradi 164 ya Sh469 bilioni yafuatiliwa

Kwa upande wake, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, alisema taasisi hiyo imefuatilia miradi 164 yenye thamani ya Sh469 bilioni, ambapo miradi 109 ilibainika kuwa na kasoro zilizohitaji hatua za ufuatiliaji ili kuhakikisha zinarekebishwa na thamani ya fedha inaendana na matokeo yaliyokusudiwa.

Ngailo alisema ukosefu wa fedha, ucheleweshaji wa utekelezaji wa baadhi ya miradi na ushiriki mdogo wa wadau ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati au kutofikia viwango vilivyokusudiwa.

Alisema changamoto hizo zinapojitokeza kwa pamoja zinaweza kuwanyima wananchi huduma na manufaa yaliyolengwa na Serikali kupitia miradi hiyo.

“Ucheleweshaji wa baadhi ya miradi, pamoja na ushiriki mdogo wa wadau, haya yote kwa pamoja yanafanya miradi hii kutekelezwa nje ya muda au ikiwa na mapungufu,” alisema Ngailo.

Alisema warsha hiyo imelenga kuwaunganisha wadau ili kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto hizo, kuongeza ushiriki wa jamii na taasisi mbalimbali katika ufuatiliaji wa miradi na kuhakikisha rasilimali zinazotengwa zinatumika kwa ufanisi.

Ngailo alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na Serikali inapata thamani halisi ya fedha inayowekeza katika miradi ya maendeleo.

“Tunategemea kwamba mikakati itakayowekwa itasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, lakini mwisho itasaidia wote kushiriki katika kusimamia miradi hii, ili tuweze kupata thamani ya fedha ambayo imekusudiwa katika uanzishaji wa miradi husika,” alisema.

Alisema kila mdau mwenye dhamana ya kusimamia, kutekeleza au kufuatilia miradi ana wajibu wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia malengo, thamani ya fedha na muda uliopangwa.

“Kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja,” alisema Ngailo.

Akihitimisha, Makalla alisema Serikali ya Mkoa wa Arusha itaendelea kushirikiana na TAKUKURU na taasisi nyingine za udhibiti kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa mujibu wa sheria, viwango na muda uliopangwa.

“TAKUKURU na taasisi zote za Serikali pamoja na watendaji tutaenda kwa pamoja kwa sababu sisi wote tunategemeana. Lengo letu ni kuhakikisha tunaongeza mapambano ya rushwa, tunaongeza uwajibikaji na kuhakikisha miradi yetu yote inatekelezwa kwa ufanisi,” alisema.

Alisema mafanikio ya warsha hiyo hayatapimwa kwa mijadala iliyofanyika pekee, bali kwa utekelezaji wa maazimio na hatua zitakazochukuliwa na kila mdau baada ya warsha hiyo.

“Tunataka TAKUKURU, Serikali na taasisi zote tufanye kazi kwa pamoja. Tukifanya hivyo tutakuwa tumesaidia kuharakisha maendeleo na kulinda fedha za wananchi,” alisema Makalla.





Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم