Breaking🔥

JIJI LA ARUSHA LATENGA BILIONI MBILI KUNG'ARISHA JIJI LA ARUSHA KWA TAA BIASHARA KUFANYIKA KWA SAA 24


ARUSHA KUWASHA TAA 500 KWA SH2 BILIONI

..Jiji lalenga usalama, biashara za usiku na uchumi wa saa 24

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

HALMASHAURI ya Jiji la Arusha imeweka Sh2 bilioni kwa ajili ya kufunga zaidi ya taa 500 za barabarani, katika hatua inayolenga kuongeza usalama, kuchochea biashara za usiku na kulifanya jiji hilo kuingia rasmi katika mpango wa uchumi unaofanya kazi saa 24.

Uamuzi huo unaifanya miundombinu ya taa kuwa miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele katika matumizi ya mapato ya ndani ya Jiji, huku Halmashauri ikisisitiza kuwa fedha zinazotokana na wananchi zinapaswa kurejea kwao kupitia huduma na miradi ya maendeleo.

Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe,akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake Agosti 5-2026, alisema Halmashauri imeendelea kutekeleza utaratibu wa kuelekeza asilimia 60 ya mapato yake ya ndani katika miradi ya maendeleo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Alisema kwa mwaka husika, Jiji linatarajia kukusanya Sh61 bilioni kupitia mapato ya ndani, huku sehemu ya fedha hizo ikielekezwa katika kuboresha miundombinu na huduma muhimu.

“Fedha hizi ni za wananchi, hivyo ni lazima wananchi waone matokeo ya kodi na michango yao kupitia miradi inayotekelezwa,” alisema.

TAA KATIKA KATA MBALIMBALI

Kwa mujibu wa Iranghe, mradi huo wa taa utatekelezwa katika kata mbalimbali za Jiji la Arusha, huku maeneo ambayo tayari yana miundombinu ya taa, yakiwamo Livolosi, Kaloleni na Sekei, yakiboreshwa zaidi.

Hatua hiyo inalenga siyo tu kuongeza mwanga barabarani, bali pia kuimarisha usalama wa wananchi wanaosafiri na kufanya shughuli zao nyakati za usiku.

Jiji linaona uwepo wa taa za kutosha kama kichocheo cha shughuli za kiuchumi baada ya muda wa kawaida wa biashara, kwa kuwa maeneo yenye mwanga na usalama huongeza uwezekano wa wafanyabiashara, wasafiri na watoa huduma kuendelea na shughuli zao hadi usiku.

BARABARA, MITARO NAYO KWENYE MIZANI

Mbali na taa, Iranghe alisema Jiji linaendelea kushirikiana na Serikali Kuu katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara, huku Halmashauri ikianza taratibu za zabuni kwa miradi mipya ya barabara za ndani.

Miradi hiyo pia inahusisha ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua, madaraja madogo na vivuko, hatua inayolenga kupunguza changamoto za usafiri pamoja na madhara yanayosababishwa na maji ya mvua katika maeneo mbalimbali ya jiji.

SH9.2 BILIONI KUTOKA KWA MAWAKALA

Katika kuongeza uwezo wa Jiji kukusanya mapato, Halmashauri imesaini mikataba na mawakala kwa ajili ya ukusanyaji wa madeni pamoja na ushuru wa maegesho ya magari.

Kupitia mikataba hiyo, zaidi ya Sh9.2 bilioni zinatarajiwa kukusanywa.

Iranghe aliwataka mawakala hao kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia masharti ya mikataba, akionya kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka taratibu au kuwatoza wananchi fedha kinyume cha sheria.

“Mawakala wakifanya vizuri wataendelea na kazi, lakini wakishindwa kutekeleza wajibu wao au kukiuka taratibu, mkataba unaweza kusimamishwa wakati wowote,” alisema.

WANANCHI WATAKIWA KULIPA KIDIJITALI

Meya huyo pia aliwahimiza wananchi kutumia njia za kidijitali, ikiwamo simu za mkononi na benki, katika kulipa kodi na tozo mbalimbali.

Alisema maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato yameongeza uwazi na kusaidia kupunguza migogoro kati ya walipakodi na mawakala.

Alisema Halmashauri itaendelea kutoa taarifa kuhusu ukusanyaji na matumizi ya mapato, ili wananchi waweze kufahamu namna fedha zao zinavyotumika katika kuboresha huduma na miundombinu.

ARUSHA KULENGA UCHUMI WA SAA 24

Uwekezaji wa Sh2 bilioni katika taa zaidi ya 500 unakuja wakati Jiji la Arusha likijipanga kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na huduma zinazoweza kuendelea hadi nyakati za usiku.

Kwa muktadha huo, taa hizo hazitazamiwi kama mradi wa kuongeza mwanga pekee, bali sehemu ya mpango mpana wa kujenga Arusha salama, yenye miundombinu bora na mazingira yatakayowezesha shughuli za kiuchumi kuendelea kwa saa 24.

Kwa Jiji linalotegemea kwa kiasi kikubwa biashara, utalii na huduma, mazingira salama ya usiku yanaweza kuwa kichocheo cha kuongeza muda wa shughuli za kiuchumi, huku ukusanyaji mzuri wa mapato ukitoa msingi wa kuendeleza uwekezaji katika miundombinu.

Mwisho.


Post a Comment

أحدث أقدم