Breaking🔥

LUKUMAY ATAKA SH584 MILIONI ZA UJENZI WA SEKONDARI MANYIRE ZITOE SHULE YA MFANO, ASIKILIZA KERO ZA WANANCHI KATA YA MLANGARINI, WAMPONGEZA WAIBUA SHANGWE KUWATEMBELEA!

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU 

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameitaka Halmashauri ya Arusha kuhakikisha Sh milioni 584 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Manyire zinatumika kwa ufanisi na kujenga shule yenye viwango vya kitaifa na kimataifa

Dkt. Lukumay ametoa agizo hilo leo, Agosti 9, 2026, wakati wa ziara yake katika Kata ya Mlangarini, ambako alitembelea mradi huo unaojengwa katika Kijiji cha Manyire.


Alisema fedha hizo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

“Lazima kuwe na uwiano kati ya kazi na fedha zilizotolewa. Hela za Serikali zionekane kwamba zimeenda kufanya kazi na inaonekana,” alisema Dkt. Lukumay.

Alisema shule hiyo inapaswa kujengwa kwa kuzingatia mahitaji ya elimu ya kisasa, akifurahishwa na mpango wa kuwa na maabara za Fizikia, Baiolojia na Kemia pamoja na maabara ya Kompyuta.

“Ningependa sekondari hii ijengwe katika viwango vya kitaifa na kimataifa. Nataka iwe shule ya kisasa kwa sababu tunaenda na mwendo wa kisasa,” alisema.

Dkt. Lukumay alisema viongozi wa Halmashauri, wahandisi na mkandarasi wanapaswa kushirikiana kwa karibu kuhakikisha ubora wa mradi unazingatiwa, huku wananchi wakishirikishwa katika usimamizi wa ujenzi huo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Lukumay aliwapongeza wananchi wa Manyire kwa kutoa ekari 14 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo bila kudai fidia kutoka Serikali.

Alisema hatua hiyo ni mfano wa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Naomba wananchi wa kata nyingine ambazo hazina sekondari waige mfano wa Manyire kwa kutoa maeneo ili Serikali iweze kujenga shule,” alisema.

Alizitaja Kata za Kiranyi na Tarakwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kujifunza kutoka Manyire katika suala la upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Mbunge huyo pia alimtaka Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, kuendelea kuwa karibu na wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hiyo.

Akizungumzia changamoto zilizowasilishwa na wananchi, Dkt. Lukumay aliwataka kutoa taarifa kwa viongozi wao na kuhakikisha kero hazibaki bila kufanyiwa kazi.

Alisema wananchi wana nafasi ya kuwasiliana naye moja kwa moja kuhusu changamoto ambazo hazijapatiwa ufumbuzi, huku akisisitiza umuhimu wa diwani na viongozi wa Serikali za mitaa kuwa mstari wa mbele kuzifuatilia.

“Wananchi msiache kutoa sauti yenu. Kama unaona chochote ambacho hakiendi vizuri, una nafasi ya kunieleza, kunipigia simu au kuniandikia ujumbe,” alisema.

Dkt. Lukumay pia aliahidi kufuatilia malalamiko ya wananchi kuhusu baadhi ya wawekezaji, akisema uwekezaji ni muhimu kwa maendeleo lakini wananchi wanapaswa kushirikishwa.

Alisema wananchi wanapewa taarifa na kushirikishwa katika maamuzi yanayohusu maeneo yao, ili kuondoa migogoro na kujenga mazingira bora ya uwekezaji.

“Tunapenda wawekezaji, lakini lazima tushirikiane kati ya wawekezaji, wananchi na Serikali kwa pamoja,” alisema.

Mbunge huyo pia aliagiza kufuatiliwa kwa madai ya wananchi kuhusu mapato yanayotokana na mashamba yaliyotangazwa na Serikali, baada ya wananchi kulalamikia kutokuwa na taarifa kuhusu fedha hizo.

Alisema wakati wa mjadala wa bajeti Bungeni alishiriki katika kueleza umuhimu wa sehemu ya mapato yatokanayo na ardhi kurejea katika Halmashauri husika kwa ajili ya maendeleo.

Dkt. Lukumay alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha kutoa taarifa kuhusu suala hilo ili aweze kulifuatilia katika ngazi husika.

“Mimi kazi yangu ni kutetea wananchi. Kwa kero kama hizi lazima tufanye kazi haraka iwezekanavyo. Hatuna muda wa kusubiri,” alisema.

Akizungumzia uwekezaji wa Serikali katika elimu, Dkt. Lukumay alisema utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo, ujenzi wa miundombinu ya shule na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuongeza fursa za elimu nchini.

Alisema uwekezaji huo umewezesha kujengwa kwa majengo mengi ya shule na kupunguza changamoto ya wanafunzi kuanza kidato cha kwanza kwa awamu kutokana na uhaba wa miundombinu.

Dkt. Lukumay aliwahimiza wananchi wa Manyire kushirikiana na viongozi kuhakikisha Shule ya Sekondari Manyire inakamilika kwa wakati na inakuwa miongoni mwa shule bora katika eneo hilo.


Ends

Post a Comment

أحدث أقدم