DIWANI MREMA AITAKA SERIKALI KUTATUA KERO ZA BARABARA, MAJI, UMEME KISERIANI
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
DIWANI wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, ameitaka Serikali kuongeza kasi ya kushughulikia changamoto za barabara, maji na umeme katika Kijiji cha Kiseriani, akisema baadhi ya miundombinu hiyo imekuwa kikwazo kwa shughuli za kiuchumi na kijamii za wananchi.
Mrema alitoa kauli hiyo Agosti 9,2026 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kitongoji cha Mbuni, Kijiji cha Kiseriani, wakati wa ziara ya Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lembulung Lukumay, aliyefika kusikiliza kero na mahitaji ya wananchi.
Alisema uongozi wa kata na kijiji umekuwa ukishirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali katika kuboresha barabara za mitaa, lakini uwezo uliopo bado hautoshelezi kukabiliana na ukubwa wa changamoto hiyo.
Alisema moja ya barabara zinazohitaji kupewa kipaumbele ni barabara ya Olmaroroi, ambayo kwa sasa imeharibika na kuwa kero kwa wananchi wanaoitumia katika shughuli zao za kila siku.
“Tunashirikiana na wadau katika kutengeneza barabara za mitaa, lakini kuna barabara ambazo ni korofi sana. Barabara ya Olmaroroi imekuwa tatizo kubwa. Tunaomba nguvu yako, Mheshimiwa Mbunge, na ukifika Bungeni uiweke kwenye mpango wako wa karibu ili ipatiwe ufumbuzi,” alisema Mrema.
Diwani huyo pia alitaja Kitongoji cha Muungano kuwa miongoni mwa maeneo yenye changamoto kubwa ya barabara, akisema baadhi ya barabara zimeharibika na zinahitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Alisema uongozi wa kata na kijiji umeendelea kuzitambua barabara hizo na kuziweka katika mipango ya maendeleo, huku wananchi wakishiriki kwa nguvu zao katika maeneo wanayoweza.
“Hata mimi pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji tunajitahidi kuendelea kuzitambua barabara hizi na kuziweka kwenye ratiba zetu, lakini nguvu yetu bado ni ndogo. Mara nyingi tunategemea wadau na wananchi wetu ambao wamekuwa wakijitolea,” alisema.
Mrema pia aliomba Serikali kupitia Mbunge huyo kuendelea kufuatilia changamoto za upatikanaji wa maji na umeme, akisema bado kuna maeneo ambayo wananchi hawapati huduma hizo kwa kiwango kinachokidhi mahitaji yao.
Alisema changamoto hizo zimekuwa zikifikishwa kwa viongozi mara kwa mara na ziara hiyo ya Mbunge imetoa fursa kwa wananchi kuzisisitiza moja kwa moja mbele ya kiongozi huyo ili hatua zaidi zichukuliwe.
Alisema wananchi wa Kiseriani wako tayari kushirikiana na Serikali, Halmashauri na wadau katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Wananchi hawa ni wapenda maendeleo na wako tayari kushirikiana kwa karibu na Serikali yao. Tunaomba Mheshimiwa Mbunge uendelee kutukumbuka Kata ya Mlangarini na kutusaidia katika kutatua changamoto hizi,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiserian, Maliaki Loisule, aliwasilisha orodha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, akitaja maji, afya, barabara, elimu pamoja na ulinzi na usalama.
Loisule alisema changamoto ya maji bado ni kubwa, huku akidai zaidi ya asilimia 85 ya maeneo ya kijiji hayapati huduma ya maji ya uhakika.
Alivitaja vitongoji vya Maloroi, Muungano, Makazi ya Mlimani na Rongima kuwa miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na tatizo hilo.
Katika sekta ya afya, alisema Zahanati ya Kiserian inahitaji ukarabati, huku kukiwa na changamoto ya nyumba za watumishi wa afya.
Alisema kutokana na ongezeko la idadi ya wananchi, kuna umuhimu wa zahanati hiyo kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya ili wananchi wapate huduma pana zaidi.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Loisule alisema kijiji kina barabara nane zenye urefu wa zaidi ya kilomita 70, ambazo kwa mujibu wake bado hazijaingizwa kikamilifu katika mipango ya matengenezo ya TARURA.
“Tunaomba barabara hizi ziingizwe kwenye mipango ya TARURA ili ziweze kutengewa bajeti na kufanyiwa matengenezo kwa utaratibu maalumu,” alisema.
Katika mkutano huo, wananchi nao walitumia fursa hiyo kueleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Elisha Laizer alilalamikia hali ya vumbi katika barabara inayofanyiwa matengenezo, akisema kutomwagiliwa maji wakati wa kazi hiyo kunasababisha vumbi kubwa na kuwaathiri wananchi.
Aliomba pia kuwekwa matuta katika maeneo hatarishi ili kupunguza kasi ya magari na pikipiki na kuzuia uwezekano wa ajali.
Naye Gilbert Mushi, mkazi wa Kitongoji cha Mbuni, alilalamikia wizi wa mita za maji, akisema tatizo hilo limekuwa likijirudia kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mushi aliomba mamlaka inayohusika na huduma ya maji kuangalia uwezekano wa kuhamisha mita kutoka nje ya nyumba na kuziweka ndani ya maeneo salama ili kupunguza uwezekano wa kuibiwa.
Kwa upande wake, Joshua Mollel alieleza changamoto ya barabara inayokwenda kwenye mgodi wa moramu uliopo katika kitongoji anachoishi.
Alisema barabara hiyo imeharibika kwa kiwango kikubwa kutokana na matumizi ya magari yanayokwenda kuchukua moramu, hali ambayo imekuwa kero kwa wananchi.
Mollel alisema hali hiyo inazua maswali kwa kuwa Halmashauri inaweka utaratibu wa kukusanya ushuru kutoka kwa magari yanayobeba moramu, lakini barabara inayotumika na magari hayo bado haijapatiwa matengenezo ya kiwango kinachostahili.
Alisema wananchi wamekuwa wakipata usumbufu kutokana na hali mbaya ya barabara hiyo na kuiomba Serikali pamoja na mamlaka husika kuchukua hatua.
Pamoja na changamoto hizo, Mwenyekiti Loisule alisema wananchi wa Kiserian wameendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa nguvu zao na kushirikiana na wadau mbalimbali.
Alisema wananchi wamechangia miradi mbalimbali, ikiwemo Sh8 milioni kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mbune–Kalemaji, huku pia wakishiriki katika shughuli za kuboresha shule na miundombinu mingine ya kijamii.
Alisema bado kuna mahitaji ya madarasa na nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Kiserian, pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa la kupikia.
Kwa mujibu wa Loisule, wananchi tayari wamechangia Sh3 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jiko hilo, lakini bado wanahitaji fedha zaidi kukamilisha mradi huo.
Katika eneo la ulinzi na usalama, aliomba Serikali kusaidia ujenzi wa Kituo cha Polisi Kiserian, akisema kijiji tayari kimetenga eneo kwa ajili ya ujenzi huo.
Loisule alisema ziara ya Dkt Lukumay ni fursa kwa wananchi kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja na kupata uwakilishi katika mamlaka za Serikali.
Alisema wananchi wanatarajia Mbunge huyo kutumia nafasi yake kufuatilia kero hizo katika mamlaka husika ili kupata ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mrema alisema uongozi wa kata utaendelea kushirikiana na wananchi na Serikali katika kuhakikisha changamoto zinazoweza kutatuliwa katika ngazi ya kata zinafanyiwa kazi, huku zile zinazohitaji nguvu kubwa zikifikishwa katika ngazi za juu.
“Wananchi hawa ni wapenda maendeleo na wako tayari kushirikiana na Serikali yao. Tunaomba Mheshimiwa Mbunge uendelee kutukumbuka Kata ya Mlangarini na kutusaidia katika kutatua changamoto hizi,” alisema.






إرسال تعليق