Breaking🔥

LUKUMAY AILIPUA HALMASHAURI: ‘MITAMBO YA BARABARA IKO WAPI?’

LUKUMAY AILIPUA HALMASHAURI: ‘MITAMBO YA BARABARA IKO WAPI?’

...Atoa muda wa siku moja, aapa kumuuliza Waziri | Aitaka Halmashauri kuacha kukalia mitambo wakati wananchi wakiteseka | Apongeza Samia kwa Sh580m za Shule ya Manyire

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU 

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameiweka Halmashauri ya Arumeru katika presha akitaka itoe majibu ya haraka kuhusu zilipo mitambo minne mikubwa ya kutengeneza barabara, huku akisema hawezi kukubali kuona wananchi wakiteseka kwa barabara mbovu wakati vifaa vya Serikali vipo.

Dkt. Lukumay ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Manyire  Kata ya Mlangarini, akisema atahitaji majibu kuhusu eneo ilipo mitambo hiyo, inafanya kazi gani kwa sasa na inaanza lini kutumika kutengeneza barabara zinazolalamikiwa na wananchi.


Amesema iwapo hatapata majibu kutoka kwa Halmashauri, atafikisha suala hilo kwa Waziri mwenye dhamana, akisisitiza kuwa yuko tayari kulifuatilia hadi majibu yapatikane.

“Tunataka tujue mitambo iko wapi, iko katika eneo gani na inaanza kufanya kazi lini. Wananchi hawawezi kuwa na mitambo mikubwa kama ile, lakini hawajui iko wapi. Niko serious kwa hili jambo,” amesema.

Mbunge huyo amemtaka Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, kuwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ili kumpatia taarifa hiyo, akisema wananchi wanahitaji kuona barabara zao zikifanyiwa kazi badala ya kuendelea kuahidiwa.

Amesema changamoto ya barabara imekuwa moja ya kero kubwa inayowakabili wananchi wa maeneo mbalimbali ya Arumeru Magharibi, hususan barabara za vijijini zinazohitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Dkt. Lukumay amesema amemtaka Mkurugenzi kuhakikisha taarifa kuhusu mitambo hiyo inapatikana haraka.

“Naomba Jumanne nipate taarifa ya mitambo. Mitambo yako wapi, iko katika eneo gani na inaanza kufanya kazi lini? Hiyo taarifa nipeleke kwa Mheshimiwa Mkurugenzi,” amesema.

Amesema kama suala hilo halitapatiwa majibu, atalazimika kulifikisha kwa Waziri wa TAMISEMI anayesimamia masuala ya barabara za TARURA ili Serikali ijue kinachoendelea.

Kauli hiyo imekuja wakati wananchi katika Kata ya Mlangarini wakiendelea kulalamikia hali ya barabara, wakitaka miundombinu hiyo iweze kupitika wakati wote ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Lukumay amewataka wananchi kuwa na matumaini kuhusu uboreshaji wa barabara ya Lawsonyiai, akisema Serikali imeanza kuchukua hatua baada ya kilio cha wananchi.

“Barabara ya Lawsonyiai imeelezwa vizuri. Imeanza kujengwa na kelele tulizopiga zimezaa matunda. Itajengwa kwa kiwango cha lami na tufurahie,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia miradi ya miundombinu inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kurahisisha shughuli zao za kiuchumi.

Kuhusu maji, mbunge huyo amewataka viongozi wa vijiji na kata kushirikiana na wananchi kulinda miundombinu ya maji, akisema vitendo vya kuiba mita vinahatarisha juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo.

Amesema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi na kushirikiana nao katika kulinda miradi ya maji ili fedha zinazotumika kujenga miundombinu hiyo zisipotee kwa vitendo vya uharibifu na wizi.

“Naomba ushirikiane na watu wa maji. Hawa watu wanaoiba mita ni hatari sana. Tukishirikiana, haya mambo yanawezekana,” amesema.

SAMIA APEWA SIFA SHULE YA MANYIRE

Dkt. Lukumay pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Sh milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Manyire, akisema mradi huo ni ushahidi wa Serikali kuendelea kuwekeza katika elimu.

Amesema ujenzi wa shule hiyo ya kisasa utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi wa eneo hilo.

“Nimshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwapenda wananchi wa kata hii na kutoa Sh milioni 580 kwa ajili ya kuwajengea shule nzuri sana ya kisasa pale Manyire,” amesema.

Katika sekta ya afya, Dkt. Lukumay amewataka viongozi wa afya kuboresha utoaji wa taarifa kwa wananchi kuhusu huduma zinazopatikana katika Hospitali ya Wilaya , Olturmenti

Amesema alipotembelea hospitali hiyo alikuta dawa zikipatikana pamoja na vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu, ikiwamo digital X-ray, maabara na vifaa vya huduma za meno.

Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa dawa na huduma, lakini walipotembelea hospitali walikuta huduma hizo zipo.

“Nilipofika hospitalini, nilipita kwenye pharmacy, dawa zote zipo. Kuna digital X-ray ambayo zamani ilikuwa inapatikana hospitali kubwa kama Mount Meru, lakini iko hapa Olturmenti,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya kuwahamasisha watumishi wa afya kuwafahamisha wananchi kuhusu huduma zinazopatikana hospitalini hapo.

“Anza kueleza watu, waeleze wananchi huduma zinazopatikana. Waeleze viongozi wa vijiji na wananchi. Hospitali ni ya kwao,” amesema.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa ubora wa huduma za afya hauishii katika upatikanaji wa dawa, bali pia namna wagonjwa wanavyohudumiwa na kupewa maelekezo.

Amesema watumishi wa afya wanapaswa kutumia muda kuwaelekeza wagonjwa namna sahihi ya kutumia dawa badala ya kutoa maelekezo mafupi ambayo yanaweza kutafsiriwa vibaya.

Amesema wananchi wanahitaji dawa, huduma bora na lugha nzuri kutoka kwa watumishi wa afya.

Dkt. Lukumay amesema mpango wa Serikali wa bima ya afya kwa wote unalenga kuhakikisha wananchi hawanyimwi huduma kwa sababu ya kukosa uwezo wa kugharamia matibabu.

Amesema utekelezaji wake unafanyika kwa awamu, huku wananchi wasio na uwezo wakipewa kipaumbele.

Ametaja watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wazee na makundi mengine yenye uhitaji kuwa miongoni mwa wanaopaswa kunufaika na huduma zinazogharamiwa na Serikali.

Pia amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika matibabu ya magonjwa sugu kama saratani, magonjwa ya moyo, figo na kisukari.

AWATAKA VIONGOZI KUWA KARIBU NA WANANCHI

Kwa upande mwingine, Dkt. Lukumay amempongeza Diwani wa Mlangarini, Emanuel Mrema, kwa kuwa karibu na wananchi na kufuatilia changamoto zinazowakabili.

Amesema viongozi wa ngazi zote wanapaswa kusikiliza wananchi na kuchukua hatua pale wanapowasilisha changamoto zao.

Ametoa wito kwa Serikali za vijiji kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kwa maendeleo ya wananchi.

“Wananchi wamewachagua kwa imani kubwa. Anzeni kufanya kazi haraka iwezekanavyo na kusimamia ukusanyaji wa mapato,” amesema.

Amesema maendeleo ya Kata ya Mlangarini yatawezekana endapo viongozi na wananchi wataendelea kushirikiana na kuhakikisha kero zinazowakabili zinafikishwa katika mamlaka husika na kufuatiliwa hadi zinapatiwa majibu.

Ends


Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم