LONGIDO YALENGA KUFIKIA MAPATO YA BILIONI 10,LEKANET ASISITIZA UTEKELEZAJI WA MAADHIMIO YA BARAZA LA MADIWANI

Longido yalenga kuvuka Sh bilioni 5.2 za mapato, yataka kufikia Sh bilioni 10

Na Joseph Ngilisho|LONGIDO. 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Longido imeweka mkakati wa kuongeza makusanyo ya mapato kutoka lengo la Sh bilioni 5.2 hadi kufikia Sh bilioni 7, 8 na ikiwezekana Sh bilioni 10, huku ikiimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato, hususan sekta ya mifugo.

Hatua hiyo imejadiliwa katika kikao cha Baraza la Madiwani, ambapo Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha , Peter Lekanet, alisisitiza umuhimu wa kuongeza mapato ili kuiwezesha Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Lekanet ambaye amethibitishwa na baraza hilo kuelelea kuitumikia nafasi hiyo kwa awamu ya pili ,alisema kiwango cha Sh bilioni 5.2 kilichowekwa kama lengo la bajeti hakipaswi kuwa mwisho wa jitihada za Halmashauri, bali kuna haja ya kuweka mikakati ya kuvuka kiwango hicho na kufikia Sh bilioni 7, 8 hadi Sh bilioni 10.

Alisema kuongezeka kwa mapato kutaiwezesha Halmashauri kuwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto mbalimbali na kutekeleza miradi inayohitajika na wananchi.

“Tunataka angalau tusikie bilioni saba, bilioni nane na hata ikiwezekana tufike bilioni kumi. Mahitaji yetu yote na changamoto tulizonazo hatuwezi kuzifikia kama hatutakuwa na uwezo mzuri wa kukusanya na kusimamia mapato,” alisema Lekanet

Makusanyo yafikia asilimia 20




Katika kikao hicho, Baraza lilielezwa kuwa hadi mwezi Agosti, mwenendo wa ukusanyaji wa mapato umefikia asilimia 20, kiwango ambacho ni zaidi ya matarajio ya awali ya takribani asilimia 16.4 kwa kipindi hicho.

Lekanet alipongeza hatua hiyo, lakini akataka Halmashauri kuendelea kukaza usimamizi wa vyanzo vya mapato ili kuhakikisha mwenendo huo unaendelea na hatimaye malengo ya juu yanafikiwa.

“Tunawapongeza wataalamu wetu kwa kazi iliyofanyika, lakini tunahitaji kuendelea kukaza. Kama lengo lilikuwa asilimia 16.4 na tumefikia asilimia 20, basi tunapaswa kuendelea kusimamia vizuri ili tufikie zaidi ya asilimia hiyo,” alisema.

Mifugo yatajwa kuwa nguzo ya mapato

Katika mjadala huo, sekta ya mifugo ilitajwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayoweza kuongeza mapato ya Halmashauri, lakini baadhi ya madiwani walieleza kuwa mfumo wa sasa wa mapato ya mifugo unaifanya Longido kubaki na sehemu ndogo ya fedha zinazokusanywa.

Madiwani walieleza kuwa Halmashauri hukusanya Sh3,000 kwa kila mbuzi na Sh7,500 kwa ng'ombe, lakini sehemu kubwa ya mapato hayo huenda Wizara ya Mifugo, huku Halmashauri ikibeba gharama za watendaji wanaohusika na ukusanyaji.

Walisema hali hiyo inahitaji majadiliano zaidi na Wizara ya Mifugo ili kuhakikisha Halmashauri yenye wananchi wengi wanaotegemea mifugo inanufaika ipasavyo na mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Akijibu hoja hiyo, Lekanet alisema tayari viongozi wa Halmashauri wamefanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo kuhusu namna ya kuhakikisha Longido inanufaika zaidi na mapato ya mifugo.

Alisema mifugo ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Longido na kwamba Halmashauri inaendelea kuchukua hatua za kuboresha usimamizi wa sekta hiyo.

Lekanet pia alisema Halmashauri imefanya mabadiliko katika eneo la mifugo, ikiwa ni pamoja na kubadilisha baadhi ya watendaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi na mapato.

Wakala kupewa nafasi kuongeza mapato

Katika mkakati mwingine, Kamati ya Fedha inayoongozwa na Ngobei imependekeza Halmashauri itangaze nafasi ya kupata wakala wa ukusanyaji wa baadhi ya mapato ili kuongeza ufanisi na ushindani katika ukusanyaji.

Lekanet alisema suala hilo limejadiliwa zaidi ya mara nne na Kamati ya Fedha kabla ya kufikia hatua ya kulifikisha Barazani kwa ajili ya kupata uamuzi.

Kwa mujibu wa Kamati, eneo linalopendekezwa kupewa wakala kwa sasa linakusanya takribani Sh1.1 bilioni, huku matarajio yakiwa kuongeza makusanyo hadi Sh3.1 bilioni.

Alisema mkataba wa wakala huyo utakuwa wa muda mfupi, usiozidi miezi sita, ili Halmashauri iweze kupima ufanisi wa mfumo huo kabla ya kuamua kama utaendelea.

Aidha, wakala atatakiwa kuweka bondi kama dhamana ya utekelezaji wa mkataba, ili kuilinda Halmashauri iwapo atashindwa kutimiza malengo yaliyowekwa.

Lekanet alisema Kamati ya Fedha itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mpango huo na kuhakikisha hatua nyingine hazichukuliwi kabla ya Kamati kujiridhisha kuhusu faida na ufanisi wa mfumo huo.

Lengo kuvuka Sh bilioni 5.2

Lekanet alisema lengo la Halmashauri si kukusanya Sh bilioni 5.2 pekee, bali kuvuka kiwango hicho na kuelekea Sh bilioni 7 au zaidi.

Alisema ongezeko la mapato litaiwezesha Halmashauri kuwa na uwezo mkubwa wa kugharamia miradi ya maendeleo, kuboresha huduma kwa wananchi na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili Longido.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya fedha, huku kila fedha inayokusanywa ikitakiwa kutumika kwa mujibu wa taratibu na kwa manufaa ya wananchi.

Lekanet aliwataka madiwani kuunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Fedha, akisema lengo la hatua hizo ni kuifanya Halmashauri ya Longido iongeze uwezo wa mapato na kutoka katika kiwango cha sasa kwenda hatua kubwa zaidi ya maendeleo.











Ends

Post a Comment

أحدث أقدم